MBUNGE NDAKIDEMI AITAKA SERIKALI KUSAMBAZA MAJI KATIKA KATA ZENYE UHABA MOSHI VIJIJINI

BUNGENI-DODOMA

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, ameendelea kuishauri Serikali kupeleka huduma ya maji safi na salama katika vijiji vinavyokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji, hasa katika kata za Mbokomu na Kimochi.

Profesa Ndakidemi alitoa hoja hiyo Mei 20,2025 alipouliza swali la nyongeza Bungeni, akitaka kufahamu mpango wa Serikali katika kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata huduma ya maji kutokana na uhaba mkubwa unaowakabili.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, alisema Serikali tayari imepokea maombi hayo na kuyajumuisha katika mipango ya wizara.

"Wakati wa maandalizi ya bajeti ya Wizara ya Maji, Mbunge Ndakidemi alitufikishia changamoto ya upatikanaji wa maji katika kata za Mbokomu na Kimochi. Tayari maeneo hayo yamewekwa kwenye mpango wa utekelezaji," alisema Mhandisi Kundo.

Aidha, alimhakikishia Mbunge huyo kuwa Serikali iko tayari kushirikiana naye kikamilifu katika kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unafanikiwa kwa maslahi ya wananchi wa Moshi Vijijini.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.