DODOMA.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, ameishauri Serikali kuanzisha programu maalum za uzalishaji wa malisho ya mifugo, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kutatua migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji nchini.Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo na Uvuvi bungeni jijini Dodoma, Profesa Ndakidemi alisema migogoro kati ya wakulima na wafugaji imeendelea kuwa tatizo sugu katika maeneo mengi ya vijijini, ambapo mara kwa mara pamekuwa na mvutano kuhusu matumizi ya ardhi.
Aliongeza kuwa uzalishaji wa malisho si tu utapunguza migogoro ya ardhi bali pia utaboresha afya ya mifugo, kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama, na hivyo kuchangia ustawi wa maisha ya wafugaji pamoja na kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.
Katika mchango wake, Mbunge huyo pia alipendekeza ujenzi wa maghala ya kuhifadhi malisho ya mifugo katika maeneo ya wafugaji, ili akiba hiyo iweze kuuzwa kwa wananchi wakati wa kipindi cha kiangazi.
“Serikali pia ianzishe skimu za umwagiliaji katika maeneo ya wafugaji ili kuwezesha uzalishaji endelevu wa malisho hata wakati wa kiangazi, sambamba na hilo, ni muhimu pia kuanzishwa kwa bima za mifugo ili kuwasaidia wafugaji wakati wa majanga,” alisisitiza.
Profesa Ndakidemi alihitimisha kwa kutoa wito kwa serikali kuangazia kwa karibu maeneo yenye migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji, na kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha amani, usalama na maendeleo endelevu katika sekta ya kilimo na mifugo.






