WAKULIMA 17,000 WANUFAIKA NA MICHE YA KAHAWA KUTOKA FLORESTA TANZANIA

MOSHI-KILIMANJARO.

Takribani wakulima 17,000 mkoani Kilimanjaro wameweza kunufaika na miche bora ya kahawa inayotolewa na Shirika la Floresta Tanzania, hatua inayolenga kuboresha uzalishaji wa kahawa na kuinua kipato cha wakulima wa maeneo ya vijijini.

Hayo yalisemwa Mei 24,2025 na Mkurugenzi wa Floresta Tanzania, Richard Mhina, wakati wa utambulisho wa mradi wa ufugaji wa nyuki, ambao unalenga kuboresha ikolojia na kuongeza kipato cha wakulima kupitia mazao yanayopatikana kutokana na ufugaji huo, mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika Wilaya ya Same, mkoani humo.

Alisema kuwa tayari vikundi 25 vya wafugaji wa nyuki vimeanzishwa katika Wilaya ya Same, lengo ni kuboresha ikolojia na kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato kupitia bidhaa mbalimbali zitokanazo na nyuki kama vile asali, nta, gundi, na maziwa ya nyuki.

Akizungumzia kuhusu kilimo cha kahawa Mhina alisema kuwa shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha kilimo bora cha kahawa kwa kushirikiana na wakulima wadogo, huku kipaumbele kikiwa ni utoaji wa miche bora na elimu ya kilimo endelevu.

“Tangu tulipoanza kugawa miche ya kahawa, zaidi ya wakulima 17,000 tayari wamenufaika na miche bora tuliyotoa kupitia Shirika la Floresta,” alisema Mhina.

Alifafanua kuwa sambamba na ugawaji wa miche hiyo, shirika pia limekuwa likitoa mafunzo kuhusu uhifadhi wa mazingira, uanzishaji wa vitalu vya miti, na matumizi ya mbinu za kisasa katika kilimo cha kahawa.

“Dhamira yetu ni kusaidia wakulima kuachana na kilimo kisichozingatia tija na kuingia katika kilimo cha biashara ambacho kitawaongezea kipato na kuboresha maisha yao,” aliongeza.

Alisema kuwa zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayochangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa, na hivyo ni muhimu kwa jamii za wakulima kulienzi na kulistawisha kwa mbinu bora.

Aidha, aliwahimiza wakulima wanaopokea miche hiyo kufuata kanuni za kilimo bora, ikiwemo kuzingatia “amri kumi za kilimo cha kahawa” zinazosaidia kuongeza tija na ubora wa mazao, pamoja na kujikinga dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo kutoka Floresta Tanzania, Joshua Bishanga, alisema kuwa uharibifu wa mazingira mara nyingi unasababishwa na ukosefu wa kipato kwa wananchi.

"Kupitia mradi wa nyuki, wananchi watawezeshwa kiuchumi na kupewa mbinu mbadala za kipato, ikiwemo kupitia upandaji wa miti ya matunda kama parachichi,"alisema Bishanga.

Kwa mujibu wa Floresta, mpango huu unaendelea kutekelezwa katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kilimanjaro, zikiwemo Same, Mwanga, Moshi Vijijini na Rombo, ambako kahawa inastawi vizuri kutokana na hali ya hewa na miinuko ya ardhi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.