NAMNA MAZIWA YA NYUKI YANAVYOFUTA MAKUNYAZI USONI NA KUKUFANYA UONEKANE KIJANA MUDA WOTE

MOSHI-KILIMANJARO.

KATIKA harakati za kutafuta tiba mbadala na njia za asili za kujikinga na magonjwa au hata kudumisha urembo, maziwa ya nyuki yameanza kuvutia hisia za wataalamu wa afya ya asili duniani.

Tofauti na mazao mengine ya nyuki kama asali na nta, maziwa ya nyuki (royal jelly) yamekuwa siri iliyofichwa kwa muda mrefu, hasa katika jamii nyingi za Kiafrika.

Maziwa haya yanatolewa na nyuki wachanga wa kike na hutumiwa kumlisha malkia wa nyuki pekee. Lishe hiyo ndiyo inayomwezesha malkia kuishi muda mrefu zaidi, kutaga maelfu ya mayai kwa siku, na kudumu na nguvu za mwili na afya ya akili kwa miaka mingi.

Wataalamu wa mazingira na afya ya asili wanataja maziwa ya nyuki kuwa miongoni mwa mazao adimu yanayochangia kuboresha afya ya ngozi, kuongeza nguvu mwilini, na kuchelewesha dalili za uzee, yakiwemo makunyazi usoni.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu faida za mazao yanayotokana na nyuki, Ofisa Mazingira kutoka Shirika la Floresta Tanzania, Judith Makange, anasema maziwa ya nyuki ni moja ya bidhaa muhimu zinazotokana na shughuli za ufugaji nyuki, lakini bado hayajafahamika sana miongoni mwa jamii.

“Wengi hujua kuwa nyuki hufugwa kwa ajili ya asali pekee, lakini kuna mazao mengine yenye manufaa makubwa, ikiwemo nta, gundi, sumu, na maziwa ya nyuki. Maziwa haya yanasaidia sana katika kuboresha afya ya ngozi kwa kuondoa makunyazi na kufanya mtu kuonekana kijana muda mrefu,” anasema Makange.

Anafafanua kuwa maziwa ya nyuki ni adimu na hupatikana kwa gharama kubwa kutokana na ugumu wa kuyavuna. Alisema lita moja ya maziwa hayo inaweza kuuzwa hadi Shilingi milioni 12, na yamekuwa yakitumiwa zaidi na watu matajiri kutoka mataifa ya Kiarabu wanaojali urembo na afya ya mwili.

Kwa mujibu wa Makange anasema, mazao hayo yana faida nyingi;  ambapo anasema asali hutumika kama chakula na tiba, nta ya nyuki hutumika kutengeneza mishumaa na vipodozi, gundi ya nyuki husaidia kutengeneza dawa, sumu ya nyuki husaidia kama tiba ya mwili.


Anasema maziwa ya nyuki hutumika kwa lishe na tiba ya ngozi, afya ya akili, na kuongeza  nguvu mwilini.

Naye Mtaalamu wa Nyuki, Kennedy Walter, anasema matumizi ya maziwa ya nyuki yameonyesha mafanikio makubwa kwa watu walio katika umri mkubwa.

Anasema watu wanaotumia maziwa hayo hata wakiwa na umri wa miaka 60, huonekana na kujihisi kama vijana kutokana na nguvu, ufanisi wa viungo, na uimara wa kumbukumbu.

“Unapotumia maziwa ya nyuki, ubongo unapata nguvu mpya, kumbukumbu hurudi, na hata mwili unarudia kuwa na nguvu za ujana, maziwa haya ni tiba ya mwili mzima,” anasema Walter.

Ameongeza kuwa maziwa hayo hutokana na lishe ya malkia wa nyuki (Queen Bee), ambaye ndiye mwenye jukumu la kutaga mayai hadi 2,000 kwa siku, na huishi muda mrefu zaidi kuliko nyuki wengine kutokana na lishe hiyo maalum.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika hilo  Richard Mhina, anasema tayari wameanzisha vikundi 25  vya ufugaji nyuki katika Wilaya ya Same  mkoani hapa, lengo likiwa ni kuboresha ikolojia na kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia mazao yanayopatikana kwa nyuki  ikiwemo, maziwa ya nyuki, asali , nta na mengineyo.

Mhina anasema shirika hilo limetoa mtaji wa mizinga 100  ambapo kila kikundi kimoja kimepata mizinga ya nyuki minne, pamoja na elimu ya namna bora ya ufugaji wa nyuki na uvunaji wa mazao yake ili kuwezesha wananchi kujiongezea kipato.

"Kabla ya kuanza kutoa mtaji wa mizinga ya nyuki katika wilaya ya Same, tayari tulishawapatia mafunzo ya ufugaji wa nyuki lakini pia na kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa hiyo ili kujipatia kipato kutokana na mazao ya nyuki,"anasema Mhina.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.