MOSHI-KILIMANJARO.
Wauguzi mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuhakikisha wanatoa huduma bora na rafiki kwa wananchi, huku wakihimizwa kutumia kaulimbiu ya mwaka huu kama mwongozo wa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya.
Hayo yameelezwa Mei 27,2025 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Jairy Khanga, katika maadhimisho ya Siku ya kwanza ya Wauguzi Duniani ambapo kwa mkoa wa Kilimanjaro yalifanyika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwenye Uwanja wa Uhuru Park.
Dkt. Khanga alisema kuwa licha ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika sekta ya afya, bado kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya wahudumu wa afya, hususan lugha zisizofaa na matumizi mabaya ya simu wakati wa kazi.
“Tumekuwa bado tunapata malalamiko. Machache kama yalivyo, yapaswa kusemwa kwa sababu ni lazima tuyapige vita,” alisema Dkt. Khanga.
“Jambo hili halikubaliki. Tunatakiwa kuzingatia utoaji wa huduma rafiki kwa wananchi wetu. Tuache kutumia muda mwingi kufanya mawasiliano binafsi wakati wa kutoa huduma,” aliongeza.
Kauli Mbiu ya mwaka 2025 inasema, "UUGUZI NGUVU YA MABADILIKO DUNIANI" ilisisitizwa kuwa inadhihirisha nafasi kubwa ya wauguzi katika kubadilisha sura ya utoaji wa huduma za afya, hasa ikizingatiwa kuwa wauguzi wanachukua zaidi ya asilimia 70 ya watumishi katika vituo vya afya nchini.
“Wauguzi ndio jeshi kubwa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Mabadiliko makubwa ya utoaji wa huduma yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na wao,” alisema Dkt. Khanga.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Katibu wa TANNA Mkoa wa Kilimanjaro, Abdallah Mkumbukwa, alieleza kuwa katika kuenzi mchango wa muasisi wa huduma za uuguzi duniani, Florence Nightingale, wauguzi wameazimia kutoa huduma mbalimbali kwa jamii.
Alisema huduma hizxo ni pamoja na uhamasishaji wa uchangiaji damu salama, upimaji wa VVU na utoaji wa elimu, huduma za chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi, upimaji wa macho, sukari, elimu ya uzazi wa mpango na shinikizo la damu.
"Huduma hizi ni sehemu ya wajibu wa wauguzi katika kuendeleza ustawi wa jamii na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya kwa wakati na kwa ubora unaostahili."alisema
Akizungumzia maendeleo ya sekta ya afya katika mkoa huo, Dkt. Khanga alieleza kuwa mkoa wa Kilimanjaro una jumla ya vituo 513 vya kutolea huduma za afya, kuanzia ngazi ya kliniki hadi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), ambapo alisema kuwa huduma sasa zinapatikana kwa uhakika, lakini ubora wake unategemea zaidi namna zinavyotolewa.
“Unaweza kuwa na huduma nzuri, lakini kama hazitolewi kwa lugha na namna rafiki, basi wananchi hawataweza kuzifikia,” alisema Dkt. Khanga.
Dkt. Khanga pia alipongeza jitihada za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, na kusema kuwa jitihada hizo zimeongeza mwitikio chanya wa wananchi kufika katika vituo vya afya.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wauguzi kutoka wilaya mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya afya, na viongozi wa serikali, yakiwa na lengo la kutambua mchango wa wauguzi katika ujenzi wa jamii yenye afya bora.