MANDAKA-MNONO
Wakulima wa kijiji cha Mandaka Mnono katika Kata ya Old Moshi Magharibi, wanakaribia kufikia ndoto ya kilimo cha uhakika, baada ya serikali kuanzisha mradi mkubwa wa umwagiliaji wa mpunga wenye thamani ya Sh bilioni 5.1.
Mradi ambao unaolenga kuimarisha uzalishaji wa mazao kwa misimu yote na hivyo kuwa suluhisho la kudumu katika kukuza kilimo na kuinua kipato cha wakulima wa eneo hilo.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, aliyasena hayo hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na halmashauri ya Moshi ndani ya jimbo lake ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mbunge Ndakidemi alisema "Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Samia Suluhu Hassan, imeonesha dhamira kubwa ya kusaidia wakulima kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huu muhimu". alisema.
"Mradi huu umekuwa ni faraja kwa wakulima wa Mandaka Mnono, wengi wao wakiishi kwa kilimo cha mvua pekee ambao mara nyingi kimesababisha mazao yao kupungua au hata kuharibika kutokana na ukame au mvua nyingi zisizotabirika.
Alisema kukamilika kwa mradi huo wa umwagiliaji wakulima watakuwa na uhakika wa maji kwa misimu yote, na hivyo kupunguza hatari ya kupoteza mazao.
“Mradi huu umekuwa mwamko mkubwa kwa familia zetu, hadi sasa tumekuwa tukilima mara moja kwa mwaka kwa sababu ya kutegemea mvua tu, lakini sasa tuna matumaini ya kuvuna mara tatu kwa mwaka,"alisema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Old Moshi Magharibi, Peter Massawe, alisema mradi huo unatarajiwa si tu kuongeza uzalishaji wa mpunga, bali pia kusaidia wakulima kupanua mazao yao na kujiongezea kipato kwa kupitia kilimo cha uhakika na kisasa.
Pia alisema kukamilika kwa mradi wa umwagiliaji utasaidia taifa kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje na kuchangia katika kufanikisha malengo ya usalama wa chakula.
Akizungumza mmoja wa wakulima wa eneo hilo Juma Mwakalebela, alisema mradi huo utakapokamilika utawezesha kuboresha maisha na kuwaletea maendeleo.
Kwa sasa wakulima wa Mandaka Mnono wana matarajio makubwa ya kuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya kilimo cha kisasa nchini Tanzania, wakijivunia kuwa miongoni mwa maeneo yanayoleta mabadiliko ya kiuchumi kupitia kilimo cha umwagiliaji.