MBUNGE NDADIKEMI AOMBA UJENZI WA KITUO CHA POLISI, HUDUMA ZA KIJAMII KATA YA MABOGINI

BUNGENI-DODOMA

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, ameendelea kuishauri Serikali kuboresha hali ya usalama na huduma za kijamii katika maeneo ya vijijini, hasa Kata ya Mabogini, kwa kuiomba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kusaidia ujenzi wa kituo cha polisi katika kata hiyo.

Akizungumza bungeni hivi karibuni wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo, Profesa Ndakidemi alieleza kuwa Kata ya Mabogini ina idadi kubwa ya watu, lakini kwa muda mrefu imekosa kituo cha polisi, jambo linalochangia changamoto za usalama kwa wakazi wake.

“Mheshimiwa Waziri, niliwahi kukuomba kusaidia ujenzi wa kituo cha polisi Mabogini, na ukaniahidi. Kata hiyo ina watu wengi na changamoto nyingi za kiusalama, hivyo nahitaji msaada wako kama Mbunge halali wa jimbo hilo,” alisema Prof. Ndakidemi.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo aliomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa eneo la Shabaha lililoko karibu na Chuo cha Mafunzo ya Polisi (CCP) Moshi, ili litumike kwa ajili ya maendeleo ya jamii, hususan ujenzi wa shule, zahanati na kituo cha huduma kwa wananchi.

“Eneo hilo linaweza kubadilisha maisha ya wananchi iwapo litapangiwa matumizi ya kijamii, nilishaliwasilisha ombi hili kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, na naomba lizingatiwe kwa manufaa ya wananchi,” aliongeza.

Profesa Ndakidemi amekuwa mstari wa mbele katika kuwasilisha hoja mbalimbali za maendeleo kwa jimbo lake, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za msingi kwa wananchi vijijini ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.