MBUNGE MOSHI VIJIJINI AITAKA POLISI KUMSAIDIA RAIS KULINDA KATIBA

BUNGENI-DODOMA

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi, ameliomba Jeshi la Polisi nchini, likiongozwa na Mkuu wake, IGP Camillus Wambura, kusimama imara katika kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kulinda Katiba na amani ya nchi.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi bungeni jijini Dodoma, Mei 26, 2025, Profesa Ndakidemi alisisitiza umuhimu wa Jeshi la Polisi kuzuia chokochoko zinazoweza kuhatarisha usalama wa taifa, hasa zile zinazotokana na ushawishi kutoka mataifa jirani.

“Tulishawahi kung’atwa na nyoka, Mheshimiwa Spika. Mwaka 1977 tulipoteza Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na chokochoko za mwanasiasa kutoka taifa jirani. Baadaye, Idd Amini naye alianza chokochoko hadi tukajikuta vitani, tusidharau ishara ndogo zinazojitokeza,  IGP na Jeshi lake wasimame imara, tumsaidie Rais kulinda Katiba na kudhibiti maadui wa ndani na nje,” alisema.

Prof. Ndakidemi pia alipendekeza kuwazuia watu wenye historia ya uchochezi kuingia nchini “Kwa mfano, Marekani ikiwa umehusika na masuala ya uchochezi, wanakuweka kwenye orodha ya ‘black list’ na hukuruhusu kuingia, nasi tufanye hivyo kwa watu waliothibitika kuwa na nia mbaya,” aliongeza.

Katika mchango wake Prof. Ndakidemi, aliomba Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kumsaidia kujenga kituo cha polisi katika Kata ya Mabogini, akieleza kuwa eneo hilo lina idadi kubwa ya watu lakini halina huduma hiyo muhimu.

“Mheshimiwa Waziri, niliwahi kukuomba kusaidia ujenzi wa kituo cha polisi Mabogini, ukaniahidi, Kata hiyo ina watu wengi na changamoto nyingi za kiusalama, hivyo nahitaji msaada wako kama Mbunge halali wa jimbo hilo,” alisema.

Kadhalika, alitoa wito kwa Serikali kutoa eneo la Shabaha lililopo karibu na Chuo cha Mafunzo ya Polisi (CCP) Moshi, kwa ajili ya ujenzi wa shule, zahanati na kituo cha huduma kwa wananchi.

Akiangazia changamoto za ajali za barabarani, Prof. Ndakidemi alishauri Jeshi la Polisi kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ya usalama barabarani.

“Tochi za kisasa ziwekwe kwenye maeneo maalum barabarani. Ziwawezeshe kupiga picha magari yanayokiuka sheria bila askari kuwepo. Taarifa hizo ziunganishwe na vitambulisho vya NIDA ili faini zitumwe moja kwa moja kwa mmiliki. Polisi ni wachache, teknolojia inaweza kusaidia,” alisisitiza.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.