MOSHI-KILIMANJARO.
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeipongeza Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kilimanjaro (Moshi RVTSC), kwa kuanzisha na kutekeleza programu jumuishi ya mafunzo ya ufundi ya teknolojia ya uchimbaji wa madini kwa kushirikiana na sekta binafsi
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, alitoa pongezi hizo Januari 7,2026, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro, baada ya kutembelea karakana za mafunzo chuoni hapo.
Akizungumza baada ya kutembelea karakana nne kati ya 18 zilizopo chuoni hapo, Naibu Waziri amesema programu ya Integrated Mining Technical Training inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya VETA na Chemba ya Madini Tanzania (TCM), imewezesha utoaji wa mafunzo yanayoendana na mahitaji halisi ya sekta ya madini nchini.
Alibainisha kuwa sekta ya madini ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa, akisema mchango wake katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 10.1 mwaka 2025, hali inayoonesha umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu wenye ujuzi.
Kutokana na mafanikio hayo Naibu Waziri Ameir aliielekeza VETA kuongeza ushirikiano na makampuni zaidi ya sekta binafsi, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na kukuza ujuzi wa teknolojia mpya zinazoendana na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za uhaba wa vifaa, miundombinu na watumishi katika vyuo vya ufundi stadi, pamoja na kuongeza fursa za mafunzo kwa wakufunzi, sambamba na uwekezaji wa ujenzi wa vyuo vipya 65 vya VETA nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Moshi RVTSC, Mhandisi Lupakisyo Mapamba, amesema chuo hicho kimeshasajili wanagenzi zaidi ya 1,578 katika fani mbalimbali za uchimbaji wa madini, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wahitimu wamefanikiwa kuajiriwa au kujiajiri ndani na nje ya nchi.
Chuo cha VETA-Moshi, ni miongoni mwa vyuo vinavyomilikiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, chuo ambacho kipo Kanda ya Kaskazini mkoa wa Kilimanjaro katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.







