MVUA ZAKATA MAWASILIANO MIKAMENI MWANGA, OFISI YA MBUNGE YATOA MSAADA WA HARAKA

MWANGA-KILIMANJARO.

MVUA kubwa zinazoendelea kunyesha katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro zimesababisha kuharibika kwa miundombinu ya barabara, hali iliyosababisha kukatika kwa mawasiliano katika Kitongoji cha Mikameni kilichopo ndani ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mwanga.

Akizungumza na wananchi wa eneo hilo kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Mwanga Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, Katibu wa Mbunge Jeremiah Boniphace Mziray; 

Alisema mvua hizo zimesababisha kusombwa kwa karavati pamoja na sehemu ya barabara inayounganisha Kitongoji hicho, hali iliyosababisha wakazi wa pande mbili kushindwa kupita na kupata huduma za kijamii.

"Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mwanga ilifika katika eneo la tukio kwa ajili ya kujionea madhara yaliyotokea na kuweka mikakati ya haraka ya kukabiliana na changamoto hiyo."alisema Mziray.

Alisema baada ya kufika katika eneo la tukio na kujionea uharibifu mkubwa uliotokea, tayari tumeanza kuchukua hatua za awali ili kurejesha mawasiliano na huduma kwa wananchi.

Alibainisha kuwa Ofisi ya Mbunge imepanga kupeleka malori mawili ya mawe ili kuanza ujenzi wa karavati hilo kwa dharura, hatua itakayosaidia kurejesha huduma za usafiri kama ilivyokuwa awali.

Aidha, Katibu wa Mbunge alichangia mifuko mitano ya saruji pamoja na binding wire, huku akiwasihi wananchi na wadau wengine kushirikiana na kutokosubiri hadi majanga yatokee.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwanga, Hanji Solomon, alisema barabara hiyo inayofahamika kama Badi Road ni ya wananchi na ilijengwa kwa nguvu za wananchi kwa kutumia mawe na gabioni, lakini imeharibiwa na maji yaliyosababishwa na mvua kubwa.

Aliongeza kuwa taratibu za kuisajili barabara hiyo tayari zimefanyika na wanatarajia kupatiwa code number ili iweze kuhudumiwa rasmi na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Aidha Diwani huyo, alimshukuru mbunge pamoja na wadau wengine kwa msaada walioutoa katika kukabiliana na changamoto hiyo, huku akisema kuwa ujenzi wa kurejesha miundombinu hiyo utaanza mara moja ili kuhakikisha huduma zinarejea kwa haraka.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.