MAKARANI WAONGOZAJI WAPIGA KURA WAASWA KUTENDA HAKI BILA UBAGUZI

MOSHI-KILIMANJARO.

MAKARANI waongozaji wapiga kura wa Jimbo la Vunjo, wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, haki na bila upendeleo wowote wakati wa Uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kirua Vunjo Magharibi.

Rai hiyo imetolewa Januari mosi, 2026 na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Vunjo, Lucas Mselle, wakati akifungua mafunzo ya makarani waongozaji wapiga kura, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Mselle amesema makarani hao wana wajibu wa kikatiba kusimamia zoezi la kupiga na kuhesabu kura kwa niaba ya Tume, akieleza kuwa dhamana waliyopewa ni nyeti na ina mchango mkubwa kwa mustakabali wa Taifa.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanawahusisha makarani 26 watakaohudumu katika vituo 24 vya kupigia kura vilivyopo Kata ya Kirua Vunjo Magharibi, ambapo mada mbili zinawasilishwa ili kuwajengea uelewa wa pamoja na kukabiliana na changamoto za uchaguzi.

Msimamizi huyo amewahimiza washiriki wapya kutumia fursa ya mafunzo hayo kujifunza kwa haraka kupitia watendaji wenye uzoefu, huku makarani wazoefu wakitakiwa kutoa ushirikiano na kuendelea kujiongezea maarifa mapya.

Aidha, amewataka makarani hao kushirikiana vyema na mawakala wa vyama vya siasa, kuepuka kuwa chanzo cha malalamiko, pamoja na kuhakiki vifaa vya uchaguzi kabla ya kuelekea katika vituo vyao vya kazi, akisisitiza kuwa watawajibika moja kwa moja kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.