DKT. NGWARU MAGHEMBE, AWASHUKURU WANANCHI WA MWANGA KWA KUMCHAGUA

MWANGA-KILIMANJARO.

MBUNGE wa Jimbo la Mwanga, Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, amewashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa imani kubwa waliyompa kwa kumchagua kuwa mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Shukrani hizo zilitolewa wakati wa kikao cha wananchi wa kijiji cha Pangaro, Kata ya Mgagao, Wilayani Mwanga, ambacho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza kwa niaba ya mbunge huyo, Katibu wa Mbunge, Jeremiah Boniphace Mziray, alisema Dkt. Maghembe anatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wananchi wa Mwanga katika ushindi huo, akieleza kuwa imani waliyoionesha itakuwa chachu ya kufanya kazi kwa bidii zaidi.

Mziray alitoa kauli hiyo baada ya kupewa fursa ya kuwasalimia wananchi wa kijiji cha Pangaro wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliyekuwa katika ziara ya kikazi wilayani humo.

Alisema kuwa ushindi wa mbunge huyo unaonesha wazi kuwa wananchi wana imani kubwa na uongozi wa CCM, pamoja na kukubalika kwa wagombea wake wa udiwani, katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

“Kwa niaba ya Mbunge Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, anawashukuru sana wananchi wa Mwanga kwa kumwamini, lakini pia kwa kuwaamini wagombea wote wa udiwani wanaotokana na CCM, jambo linaloonesha chama kinakubalika na wananchi wake,” alisema Mziray.

Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa mbunge huyo ataendelea kushirikiana nao bega kwa bega katika kutatua changamoto za maendeleo, ikiwemo miundombinu, huduma za kijamii na ustawi wa wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wao, wananchi wa kijiji cha Pangaro Rombo Mareki, Joel Imani na Julias Moses, walieleza matumaini makubwa kwa mbunge huyo, wakisema wanatarajia kuona maendeleo zaidi yakiletwa katika maeneo yao kupitia ushirikiano wa karibu kati ya viongozi na wananchi.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.