MWANGA.
SERIKALI ya Mkoa wa Kilimanjaro imemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mwanga kuhakikisha kijana anayehusishwa na kumpa ujauzito binti aliyefanikiwa kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka ujao anatafutwa popote alipo na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, wakati akizungumza na uongozi wa Wilaya ya Mwanga katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa amepokea taarifa za kuwepo kwa mwanafunzi wa kike aliyepata ujauzito licha ya kuchaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza, hali aliyoieleza kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za mtoto na kikwazo kwa maendeleo ya elimu.
“Kuna taarifa ya mtoto wa kike aliyechaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka ujao kupewa ujauzito, yule aliyempa mimba hakikisheni anapatikana haraka na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Nurdin Babu.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwataka Wakuu wa Wilaya zote mkoani Kilimanjaro kuhakikisha watoto wote walioandikishwa kuanza elimu ya awali na msingi wanaripoti shuleni ifikapo Januari 13, 2026, bila kikwazo chochote.
Alisisitiza kuwa watoto wote walioandikishwa kuanza darasa la kwanza, pamoja na wale waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza, wanapaswa kuripoti shuleni kwa wakati, akibainisha kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya elimu na haitavumilia uzembe au vitendo vinavyowanyima watoto haki yao ya msingi ya elimu.
Mkuu wa mkoa yuko Wilayani Mwanga kwa ziara ya kikazi ya kusikiliza kero na changamoto za wananchi pamoja na kuzitafutia ufumbuzi, akiwa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa.







