MOSHI-KILIMANJARO.
DIWANI wa Kata ya Msaranga, Alhaji Ally Pendo, amesema changamoto ya miundombinu hususan vivuko vya watembea kwa miguu imekuwa miongoni mwa matatizo makubwa yaliyokuwa yakikabili kata yake.
Akizungumza Januari 12, 2026 wakati wa makabidhiano ya kivuko hicho kwa wananchi, Diwani Pendo alisema ujenzi wa kivuko hicho ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake ndani ya siku 100 tangu alipoapishwa kuwa diwani wa kata hiyo.
Alisema kivuko hicho kinalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi, huku kikiziunganisha Kata ya Msaranga na Kata ya Ng’ambo ambazo hutegemeana katika huduma mbalimbali.
Diwani Pendo alieeleza kuwa wanafunzi wengi kutoka Kata ya Ng’ambo husoma Msaranga na awali walikuwa wakikumbana na changamoto kubwa ya kuvuka mto hasa kipindi cha masika, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wao.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ng’ambo, Gadiel Mrema, alisema kwa takribani miezi minane wananchi walishindwa kuwasiliana baada ya kivuko cha awali kusombwa na mafuriko, na kuiomba serikali kujenga kivuko cha kudumu.
Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mnazi, Damas Ngowi, alisema wanafunzi walikuwa wakilazimika kuamka alfajiri na kuzunguka umbali mrefu kufika shule kutokana na kukosekana kwa kivuko salama.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Stephano Masaoe, alisema tatizo hilo limekuwepo kwa muda mrefu na limekuwa likiwaathiri zaidi wanafunzi hususan msimu wa mvua ambapo korongo hujaa maji na kuhatarisha usalama wao.
Nao Wanafunzi wanaosoma shule ya msingi na sekondari katika kata hizo Pascal Ruben, Edward Nicholaus na Elibariki Ngowi walisema walikuwa wakilazimika kuvuka mto kwenda shule na nyakati za mvua walishindwa kabisa kuvuka kwa hofu ya kusombwa na maji, hali iliyowalazimu kurejea nyumbani.
Baadhi ya wakazi na wazazi wameishukuru uongozi kwa ujenzi wa kivuko hicho wakisema kimeokoa usalama wa watoto wao, huku wakiomba serikali kuweka kivuko imara katika eneo la Makiro ili kuondoa kabisa changamoto ya kuvuka kipindi cha mvua.












