MOSHI-KILIMANJARO.
UONGOZI wa Hospitali Teule ya St. Joseph umetakiwa kuweka bei rafiki za huduma za afya ili kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kupata huduma za matibabu bila vikwazo vya gharama.
Mbunge Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Mohamed Shayo, aliyasema hayo Januari 13, 2026, wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la wagonjwa wa dharura katika Hospitali teule ya St. Joseph iliyoko Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, akisema wananchi hutofautiana kwa vipato, hivyo huduma za afya zinapaswa kuzingatia hali halisi ya maisha ya watu.
Shayo alisema kuwepo kwa bei nafuu kutawafanya wananchi wengi zaidi kukimbilia hospitalini mapema wanapougua au kupata ajali, hali itakayosaidia kuokoa maisha na kupunguza madhara makubwa ya kiafya.
Alisema huduma za dharura ni nguzo muhimu katika sekta ya afya kwa kuwa huokoa maisha ya watu wanaokumbwa na ajali na magonjwa ya ghafla, na kwamba ujenzi wa jengo hilo utaongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za haraka, salama na zenye viwango vya juu vya kitaaluma.
Aidha aliipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya nchini, ikiwemo kuongeza ajira kwa watumishi wa afya, kuboresha miundombinu na kuweka mazingira bora ya kazi, hatua zilizosaidia kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo aliwataka wahudumu wa afya kuhakikisha jengo hilo linatunzwa ipasavyo na huduma zinazotolewa zinazingatia maadili ya taaluma, huruma, utu na heshima kwa wagonjwa wote wanaofika hospitalini hapo.
Awali akisoma taarifa ya kitaalamu, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya St. Joseph, Sister Dkt. Hellen Benedict Kyilyosudu, alisema ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura umetokana na ongezeko la idadi ya wagonjwa, ambapo mradi huo umegharimu jumla ya shilingi milioni 467.5, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.
Hospitali Teule ya St. Joseph–Soweto ni hospitali ya Kanisa iliyopo katika Jimbo Katoliki la Moshi, inayomilikiwa na kuendeshwa na Masista wa Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro kwa ubia na Serikali.




.jpg)

