DIWANI WA KATA YA KIUSA AKAGUA ZOEZI LA UANDIKISHAJI WA WANAFUNZI, APOKEA CHANGAMOTO ZINAZOZIKABILI SHULE

MOSHI-KILIMANJARO.

DIWANI wa Kata ya Kiusa HalmashauriyaManispaaya Moshi, Khalid Shekoloa, amefanya ziara katika shule zilizopo ndani ya kata yake kwa lengo la kukagua maendeleo ya elimu, hali ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali, darasa la kwanza pamoja na kidato cha kwanza, sambamba na kusikiliza changamoto zinazozikabili shule hizo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Diwani Shekoloa alisema ametembelea shule tatu ambazo ni Shule ya Msingi Jamhuri, Shule ya Msingi Muungano na Shule ya Sekondari Kiusa, ambapo alieleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wazazi katika kuwaandikisha watoto wao shuleni.

Alisema mwitikio huo umewezesha shule nyingi kufikia malengo ya uandikishaji yaliyokuwa yamepangwa kwa mwaka huu wa masomo.

“Nawashukuru sana wazazi kwa namna walivyojitokeza kwa wingi kuwaandikisha watoto wao shuleni,” alisema Shekoloa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Jamhuri, Salome Ngotti, alisema shule hiyo ambayo ni kongwe inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya madarasa, uhaba wa kompyuta kwa ajili ya wanafunzi pamoja na upungufu wa vyoo.

Ngotti aliongeza kuwa serikali tayari imeipatia shule hiyo fedha kiasi cha shilingi milioni 6.3 kwa ajili ya ujenzi wa matundu mawili ya vyoo pamoja na shimo, hatua aliyoitaja kuwa ni msaada mkubwa katika kuboresha mazingira ya shule.

Akizungumzia hali ya uandikishaji, Ngotti, alisema shule hiyo tayari imewapokea wanafunzi 31 wa darasa la awali kati ya 60 waliotarajiwa, huku wanafunzi 58 wa darasa la kwanza kati ya 80 wakiwa wameshaandikishwa.

Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Muungano, Athuman Msuya, alisema changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo ni uhaba wa maji, hali inayokwaza shughuli za kila siku za shule, hata hivyo, aliishukuru serikali kwa maboresho ya miundombinu yaliyofanyika katika shule hiyo.

Mkuu wa shule ya sekondari Kiusa Mariagoreth Maliga, alisema shule hiyo, inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa, jiko la kupikia chakula cha wanafunzi pamoja na uhaba wa madawati takribani 200, hali inayowalazimu wanafunzi kukaa kwa kubanana wakati wa masomo.

Katika ziara yake hiyo Diwani Shekoloa alisema, amezipokea changamoto zote zilizowasilishwa na walimu wa shule za msingi na sekondari, akibainisha kuwa atazifikisha katika mamlaka husika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Kata ya Kiusa.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.