MWANGA-KILIMANJARO.
MBUNGE wa Jimbo la Mwanga, Dk. Ngwaru Maghembe, ameanza ziara maalum ya kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao Bungeni katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.
Ziara hiyo inalenga kuwashukuru wananchi, kusikiliza na kutatua kero zao, pamoja na kuanza utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni, katika ziara hiyo, mbunge anaambatana na viongozi wa Chama na Serikali katika ngazi mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Mbunge huyo, Jeremiah Boniphace Mziray, ziara hiyo imeanza rasmi leo Januari 16, mwaka huu, ambapo siku ya kwanza mbunge ameanza katika Kata ya Kileo.
Akiwa katika kata hiyo, Dkt. Maghembe anatarajiwa kufanya kikao cha ndani na viongozi wa Chama na Serikali pamoja na wazee, kabla ya kufanya mkutano wa hadhara mchana katika eneo la Kituri.
Baada ya hapo, mbunge na msafara wake wataelekea Kata ya Lang’ata, ambako pia atafanya kikao cha ndani na viongozi husika na baadaye kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.
![]() |
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kesho, Januari 17, mbunge ataendelea na ziara yake katika Kata ya Toroha, ambapo atakutana na wazee pamoja na viongozi wa Chama na Serikali kwa mazungumzo ya ndani, kabla ya kufanya mkutano wa hadhara mchana.
Baada ya hapo, msafara huo utaelekea Kata ya Kwakoa, ambako mbunge atafanya kikao cha ndani na viongozi na kisha kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwa lengo la kuwashukuru kwa kumuamini na kumchagua kuwa mwakilishi wao Bungeni.
Aidha, Januari 18, Dkt. Maghembe anatarajiwa kuwa katika Kata ya Mgagao, ambapo atafanya kikao cha ndani na wazee pamoja na viongozi, kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Katibu wa Mbunge amesema kuwa ndani ya siku 100 za kwanza za uongozi wake, Dkt. Maghembe amedhamiria kufika katika kata zote 20 za Jimbo la Mwanga ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Amesema tayari mbunge ameanza utekelezaji wa azma hiyo kwa kufika Kata ya Kivisini, ambako alikabidhi mipira ya maji katika Kijiji cha Kitogoto, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa kijiji hicho.







