MAJI YAIBUKA MADARASANI SHULE YA MSINGI MNOA, WANAFUNZI HATARINI .



KILEO-MWANGA

CHANGAMOTO kubwa ya maji kuibuka katika Shule ya Msingi Mnoa, iliyopo Kijiji cha Kileo Wilayani Mwanga, imeendelea kuwasumbua wanafunzi na walimu, hali inayohatarisha usalama wa majengo ya shule na maisha ya wanafunzi.

Akizungumza jana katika kikao cha hadhara kilichofanyika Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Kileo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Philipo Samson, alisema maji huibuka ndani ya vyumba vya madarasa, vyoo pamoja na jengo la utawala, hali inayowalazimu walimu kufundisha wakiwa wamekanyaga maji.

Alisema hali hiyo imefanya vyoo vya shule kudidimia na kuongeza hatari ya majengo ya shule kuanguka, licha ya jitihada za kijiji kuchimba mifereji ya kupitisha maji hayo kushindikana.

Kutokana na changamoto hiyo, kijiji kimeanza kutafuta eneo jingine ili Serikali iweze kujenga shule mpya, huku kikitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kuzuia madhara kwa wanafunzi.


Katika kikao hicho, Samsoni pia aliwasilisha changamoto ya ukosefu wa hosteli katika Shule ya Sekondari Kileo pamoja na uharibifu wa barabara ya kutoka Kileo hadi Kivukini mashambani, uliosababishwa na magari makubwa yanayobeba mazao.


Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Kileo, Rista Sumpa, alisema maji hayo yanatokana na chemchemi inayojitokeza wakati wa msimu wa mvua, akibainisha kuwa hali hiyo ni hatari kwani majengo ya shule yanaweza kuzama.

Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Dkt. Ngwaru Maghembe, alisema amezipokea changamoto zote zilizowasilishwa na kuahidi kuzifanyia kazi, akisisitiza kuwa yupo jimboni kwa ziara ya kuwashukuru wananchi na kusikiliza kero zao.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.