LANG’ATA-MWANGA.
NAIBU Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, amewaahidi wakazi wa Kata ya Lang’ata kupatikana kwa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Lang’ata, akisema ni miongoni mwa vipaumbele vyake kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa haraka na usalama.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo wakati wa ziara yake ya kuwasikiliza na kuwashukuru, Dkt. Ngwaru, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga, alisema hatapumzika hadi kituo hicho kipate gari la wagonjwa pamoja na maboresho ya miundombinu na vifaa vya tiba.
“Sitapumzika hadi Kituo cha Afya Lang’ata kipate gari la wagonjwa na huduma ziimarishwe,” alisema.
Aidha Dkt. Ngwaru alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ahadi ya kutenga Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa vikundi maalum kupitia halmashauri.
Alisema mikopo hiyo, itakapoanza kutolewa atahakikisha inawafikia walengwa bila urasimu wowote ili iwe chachu ya maendeleo kwa wananchi, hususan vijana, wanawake na makundi maalum.
Akijibu kero iliyowasilishwa ya wananchi wa kata hiyo kutokuwq na Utambulisho wa Taifa wa (NIDA), Dkt. Ngwaru alisema ofisi yake imeichukua changamoto hiyo.
Kuhusu changamoto ya umeme, alisema atafuatilia kwa karibu kuhakikisha vitongoji vyote ambavyo bado havijaunganishwa na umeme vinafikiwa na huduma hiyo, akisisitiza kuwa ndani ya kipindi chake cha ubunge hakutakuwa na kitongoji chochote kisicho na umeme.
“Ndani ya kipindi changu sitaki kuona kitongoji kisicho na umeme. Wananchi mtakuwa mkiangalia televisheni kama Watanzania wengine,” alisema.
Katika mkutano huo, wananchi wa Kata ya Lang’ata waliwasilisha kero mbalimbali zikiwemo changamoto za Kituo cha Afya Lang’ata, uhaba wa vifaa vya tiba, miundombinu mibovu ya barabara, pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.
Wananchi pia walilalamikia ushuru wa samaki wa shilingi 2,000 kwa kila ndoo, wakiomba upunguzwe hadi shilingi 1,000 ili kuwawezesha wavuvi wengi kulipa kwa hiari na kuondokana na matumizi ya njia zisizo rasmi.
Vilevile, waliomba kupatiwa maafisa wa uvuvi, kilimo na maendeleo ya jamii, wakieleza kuwa kwa zaidi ya miaka kumi Kata ya Lang’ata imekuwa haina wataalamu hao muhimu kwa maendeleo ya wananchi.





