MIKOPO YA ASILIMIA 10 YAWAINUA WATU WENYE ULEMAVU MOSHI

MOSHI-KILIMANJARO

ZAIDI ya vikundi 84 vya watu wenye ulemavu, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi vimenufaika na mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Sh milioni 277.5 iliyotolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri tangu mwaka 2021, hatua ambayo wanufaika wanasema imewawezesha kujitegemea kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

Wanufaika hao walitoa shukrani zao kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan wakisema uamuzi wa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya makundi maalumu umefungua fursa kwa watu wengi wenye ulemavu kuanzisha na kukuza biashara, kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa hafla ya kukabidhiwa mikopo hiyo, walieleza kuwa tofauti na ilivyokuwa awali, sasa wana uwezo wa kupata mitaji kwa urahisi bila vikwazo vya dhamana wala riba, jambo lililowajengea imani ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.

Mkazi wa Kata ya Bondeni, Salvatori Kombe, mwenye ulemavu wa viungo, alisema mkopo wa kwanza wa Sh milioni 2.5 aliurejesha kwa wakati, hatua iliyomwezesha kupata mkopo mwingine wa Sh milioni 6.3 atakaoutumia kununua mashine ya kisasa ya kushonea viatu pamoja na malighafi za ngozi ili kupanua shughuli zake za ufundi.

"Nilikopa Sh milioni 2.5 nikafanikiwa kuurejesha kwa wakati. Leo nimeaminiwa tena kwa mkopo wa Sh milioni 6.3 ambao utanisaidia kununua cherehani ya kisasa na kuongeza uzalishaji wa biashara yangu ya viatu," alisema.

Naye Asia Saidi, mkazi wa Majengo na mmoja wa wanufaika, alisema mikopo hiyo imeondoa changamoto ambazo watu wenye ulemavu walikuwa wakikumbana nazo walipokuwa wakitafuta mitaji kutoka kwa watu binafsi.

"Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kutufungulia dirisha hili la mikopo. Zamani ilikuwa vigumu kukopeshwa kwa sababu wengi walikuwa hawaamini kama tunaweza kurejesha fedha. Leo nasi tumepata fursa ya kujenga uchumi wetu," alisema.

Kwa upande wake, Graceana Muro wa Kata ya Mji Mpya alisema hakuwahi kutarajia kupata mkopo usio na riba kwa urahisi, akibainisha kuwa fedha hizo zitamwezesha kupanua biashara yake na kuongeza kipato cha familia.

Diwani wa Kata ya Kaloleni, Nasibu Mariki, alisema utoaji wa mikopo hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayozielekeza halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aliwataka wanufaika kuhakikisha wanaitumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuirejesha kwa wakati ili iweze kuwafikia wananchi wengine wenye uhitaji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, alisema tangu mwaka 2021 hadi Juni 2026 halmashauri hiyo imetoa mikopo ya Sh milioni 277.527 kwa vikundi 84 vya watu wenye ulemavu.

Alisema mikopo hiyo imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kujitegemea kiuchumi, kuanzisha na kukuza biashara pamoja na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo ya Manispaa ya Moshi.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.