MOSHI-KILIMANJARO.
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kaskazini imeanza mchakato wa kuanzisha Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa wafungwa, hatua inayolenga kuwajengea ujuzi wa kazi, kurekebisha tabia zao na kuwawezesha kujitegemea kiuchumi baada ya kumaliza kutumikia vifungo vyao.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kaskazini, Monica Mbelle, aliyasema hayo jana, wakati wa kikao cha pamoja kati ya VETA Kanda ya Kaskazini na Jeshi la Magereza kilichofanyika katika Makao Makuu ya VETA Kanda ya Kaskazini, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Alisema ushirikiano huo ni mwanzo muhimu wa kuanzisha programu itakayowawezesha wafungwa kupata ujuzi wa ufundi stadi unaohitajika katika soko la ajira na kujiajiri.
Mbelle alisema jukumu la VETA ni kutoa mafunzo yanayowawezesha vijana na makundi mbalimbali ya jamii kupata ujuzi wa kazi, hivyo kuwasaidia kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya taifa.
"Tunapounganisha nguvu kati ya VETA na Jeshi la Magereza, tunalenga kuwapatia wafungwa ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi na kujipatia kipato, ninaamini mpango huu utawanufaisha wafungwa binafsi, utaongeza uzalishaji ndani ya Jeshi la Magereza na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla," alisema Mbelle.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkuu wa Gereza Kuu Karanga, Mkaguzi wa Magereza Godfrey Madegwa, aliishukuru VETA Kanda ya Kaskazini kwa utayari wake wa kushirikiana na Jeshi la Magereza katika kutekeleza jukumu la kurekebisha tabia za wafungwa kupitia mafunzo ya ufundi stadi.
Alisema lengo la Jeshi la Magereza si kuwaadhibu wafungwa pekee, bali pia kuwaandaa kuwa raia wema wenye uwezo wa kujitegemea wanaporejea katika jamii baada ya kutumikia vifungo vyao.
"Mfungwa anapomaliza kifungo hukutana na changamoto za kukubalika na kuaminiwa na jamii, kupitia mafunzo haya ya ufundi stadi, tunawajengea uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji na kujipatia kipato, jambo litakalowasaidia kuanza maisha mapya kwa heshima na kujitegemea," alisema Madegwa.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatawapa wafungwa ujuzi wenye tija utakaowawezesha kushiriki katika shughuli za uzalishaji, kupunguza utegemezi na kuongeza nafasi ya kujenga maisha bora baada ya kutoka gerezani.
Ushirikiano kati ya VETA Kanda ya Kaskazini na Jeshi la Magereza unatarajiwa kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa wafungwa kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na fursa za kujiajiri, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wanarejea katika jamii wakiwa na ujuzi, nidhamu na uwezo wa kujitegemea.




