WANANCHI WA VIJIJI VYA KILINGA, NKOANEKOLI WALIOTUNZA CHEMCHEMI YA MAJI, WANATARAJIWA KUNUFAIKA NA MAJI

ARUMERU-TANZANIA.

BODI ya Maji Bonde la Pangani imewapongeza wananchi wa vijiji vya Kilinga na Nkoanekoli vilivyopo Kata za Songoro na Nkoanekoli, Wilayani Arumeru kwa juhudi zao za kuendelea kulinda vyanzo vya maji.

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Mhandisi Segule Ally Segule, ameyasema hayo, baada ya kutembelea chanzo kipya cha chemchemi cha maji kilichoko Kijiji cha Kilinga;

Ambacho kimetunzwa kwa zaidi ya miaka 60, huku akiahidi kufanya tathmini ya kitaalamu ili kuona uwezekano wa kuwapatia huduma ya maji safi na salama kupitia chemchemi mpya iliyogunduliwa katika eneo hilo.

Katika ziara hiyo ya watafiti wa maji chini ya ardhi kutoka Bodi ya Maji Bonde la Pangani, waliambatana pia na viongozi wa kijiji na Kata ya Nkoanekoli hadi katika chemchemi hiyo mpya ambapo walitembea umbali kilometa 9.6 hadi kufika katika chanzo hicho ambacho kipo ndani ya msitu mnene.

Segule alisema bodi hiyo imevutiwa na namna wananchi walivyohifadhi chemchemi hiyo tangu mwaka 1963 bila kuharibu mazingira yanayoizunguka.

Mhandisi Segule alisema wataalamu tayari wameanza kufanya vipimo vya kiwango cha maji kinachotoka kwenye chemchemi hiyo ili kubaini uwezo wake wa kuhudumia wananchi, akisisitiza kuwa wananchi waliokihifadhi chanzo hicho kwa miaka mingi wanapaswa kuwa wa kwanza kunufaika endapo mradi wa maji utatekelezwa.

Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Kilingi, Elisonguo Gabriel Shoo mwenye umri wa miaka 79, alisema aligundua chemchemi hiyo mwaka 1963 wakati wa kiangazi na tangu hapo amekuwa akiilinda huku akiruhusu wananchi kutumia maji kwa matumizi ya nyumbani. 

Naye Diwani wa Kata ya Nkoanekoli, Nicodem Mbise, alisema licha ya kata hiyo kuwa na vyanzo tisa vya maji vinavyohudumia maeneo mbalimbali, wananchi wengi bado wanakabiliwa na uhaba wa maji kutokana na gharama kubwa za kusukuma maji kwa kutumia pampu za umeme.

Alisema matumizi ya chemchemi hiyo yatasaidia kupunguza gharama na kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Baadhi ya viongozi akiwamo Eliud Nnko, Mwenyekiti wa CCM tawi la Nkoanekoli Clement Kaaya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji kijiji cha Nkonekoli Danfred Emanuel, walisema, wamekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji , hivyo wanamatumaini ya kupata maji tiriri yenye uhakika.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.