MOSHI-KILIMANJARO
TIMU ya Green Eagle FC imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Zuberi Cup baada ya kuiondoa Ng'ambo United FC kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia mchezo wa kusisimua uliochezwa katika Uwanja wa Railway Njoro, mjini Moshi.
Katika mchezo huo wa hatua ya 16 bora, timu hizo zilitoshana nguvu kwa dakika 90 za muda wa kawaida na kulazimika kuongezewa muda ili kumpata mshindi.
Ng'ambo United ilionekana kuwa karibu kutinga hatua inayofuata baada ya mshambuliaji wake, Said Omland, kuifungia timu hiyo bao katika dakika za nyongeza.
Hata hivyo, Green Eagle FC haikukata tamaa, dakika mbili kabla ya filimbi ya mwisho ya muda wa nyongeza kupulizwa, mshambuliaji Ally Bundala aliisawazishia timu yake bao muhimu lililorejesha matumaini na kulazimisha mshindi kupatikana kwa mikwaju ya penalti.
Katika hatua hiyo, Green Eagle FC ilionyesha utulivu na umakini mkubwa, ikishinda kwa penalti 4-3 na hivyo kufuzu rasmi robo fainali ya michuano hiyo, huku Ng'ambo United ikimaliza safari yake katika hatua ya 16 bora.
Akizungumza baada ya mchezo, Kocha wa Ng'ambo United, Sufian Mganga, alisema chanzo cha kupoteza mchezo huo ni wachezaji wake kushindwa kudumisha umakini katika dakika za mwisho, jambo lililowapa nafasi wapinzani kusawazisha na baadaye kushinda kwa penalti.
Kwa upande wake, Kocha wa Green Eagle FC, Pius Raphael, alisema mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa na wenye kuvutia, akieleza kufurahishwa na ushindi huo uliowapa tiketi ya kuingia robo fainali.
Hadi sasa, timu 16 zimekuwa zikishiriki hatua ya mtoano ya Zuberi Cup, huku Green Eagle FC ikiwa timu ya kwanza kufuzu robo fainali baada ya kuiondosha Ng'ambo United katika pambano hilo lililokuwa na ushindani mkubwa.










