MAKABURI YA NJORO YAJAA, WANANCHI WAANZA KUZIKA NYUMBANI

MOSHI-KILIMANJARO.

KUJAA kwa makaburi ya Njoro, yaliyotengwa rasmi kwa ajili ya maziko katika Manispaa ya Moshi kumesababisha baadhi ya wananchi kuanza kuzika ndugu zao katika maeneo ya makazi yao, hali inayozua wasiwasi kuhusu afya ya jamii na mipango miji.

Akizungumza katika kikao cha utekelezaji wa shughuli za maendeleo, Diwani wa Kata ya Miembeni, Haruna Mushi, alisema Makaburi ya Njoro yameshindwa kukidhi mahitaji ya wakazi wa kata za Miembeni, Mjimpya, Majengo na Njoro, na kwamba baadhi ya wananchi sasa wanazika majumbani au kutumia utaratibu wa kuzika zaidi ya mwili mmoja katika kaburi moja (double decker).

Mbali na changamoto ya makaburi, Mushi aliwasilisha pia hoja kuhusu ubovu wa miundombinu ya barabara, upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi, pamoja na ukosefu wa kituo cha polisi na zahanati katika kata hiyo.

Mkazi wa Kata ya Njoro, Ashraf Khatibu Ramadhan, alikiri kuwa makaburi hayo yamejaa, akisema kwa upande wa Waislamu wana utaratibu wa kutumia upya makaburi ya zamani kwa kuchimba na kuyahamisha masalia ya mifupa kisha kuyazika pembeni kabla ya kumzika marehemu mwingine.

“Kwetu sisi hilo ni jambo la kawaida, lakini kwa upande wa ndugu zetu Wakristo sina uhakika na utaratibu wao,” alisema Ashraf.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembeni, Dyangala Abdallah Mnindwa, makaburi hayo yanahudumia kata nne na kwa sasa yamejaa kupita kiasi, huku wakati mwingine wakichimba na kukutana na miili miwili hadi mitatu katika kaburi moja.

Alisema kwa Waislamu utaratibu wa kuhamisha masalia huruhusu kaburi kutumika tena, lakini kwa baadhi ya madhehebu ya Kikristo ni changamoto, akibainisha kuwa waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa sasa hawaziki tena hapo, huku baadhi ya Wasabato na Wakatoliki wakiendelea kutumia makaburi hayo.

Mnindwa alisema serikali iliwahi kuelekeza maziko yafanyike Mtakuja, Wilaya ya Moshi Vijijini, umbali wa takribani kilometa 40, lakini wananchi walipinga kutokana na gharama na umbali huo, hali iliyochangia baadhi kuamua kuzika majumbani.

 Aliongeza kuwa mradi wa barabara unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mpango wa TACTIC unapita eneo hilo na unatarajia kufukua zaidi ya makaburi 70 kupisha ujenzi.

Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, alisema changamoto zimepokelewa na zitajadiliwa katika Baraza la Madiwani kulingana na uwezo wa bajeti, huku wananchi wakisisitiza haja ya kutengwa kwa eneo jipya la makaburi karibu na mji ili kupunguza mzigo uliopo sasa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.