MOSHI-KILIMANJARO.
BODI ya Kahawa Tanzania, TCB, imeanza kutekeleza mkakati maalum wa kitaifa wa kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini hadi kufikia tani laki tatu.
Hatua hiyo inakuja kufuatia uzinduzi wa ugawaji wa miche bora ya kahawa chotara kwa wakulima wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Uzinduzi huo umefanyika katika kijiji cha Kiruweni, kata ya Mwika Kusini, halmashauri ya Moshi, ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ambapo aligawa miche 534,000 kutoka bodi ya TCB.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa TCB, Primus Kimaryo, amesema matumizi ya miche hiyo bora yamepunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima kwa takribani asilimia 40.
Alisema kuwa miche hiyo imefanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania, TaCRI, na mkulima anashauriwa kuwa na angalau miche 540 ili kupata manufaa ya kiuchumi.
Kwa upande mwingine, Kimaryo amebainisha kuwa mwitikio wa wakulima mkoani Kilimanjaro bado ni mdogo licha ya miche hiyo kugawiwa bure na kwamba hali hiyo ni tofauti na mkoa wa Kagera ambako mahitaji ya miche hiyo yamekuwa makubwa zaidi.
Akizindua ugawaji wa miche hiyo ya kahawa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amewataka maafisa kilimo kwenda mashambani kuwasaidia wakulima moja kwa moja.
Aidha Serikali mkoani humo imepiga marufuku ukataji wa miche ya kahawa, ikisisitiza umuhimu wa kulinda zao hilo.

















