MOSHI-KILIMANJARO.
WAKULIMA wa zao la kahawa wametakiwa kujenga tabia ya kupima afya ya udongo kabla ya kutumia mbolea, ili kuongeza tija ya uzalishaji.
Ushauri huo ulitolewa Macho 30,2026 na Afisa Ugani, Rehema Siwakwi, wakati wa zoezi la ugawaji wa miche bora ya kahawa chotara 534,000 kwa wakulima wilayani Moshi.
Alisema udongo ni msingi wa uzalishaji, hivyo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini aina ya virutubisho vinavyohitajika.
Alieleza kuwa bila kupima udongo, wakulima hutumia mbolea kiholela jambo linalopunguza mavuno na kuathiri tija, na kwamba mkulima hawezi kupata mavuno bora, kama kilo tano kwa mche mmoja, iwapo afya ya udongo haitazingatiwa.
Katika hatua nyingine, Afisa Kilimo huyo aliishukuru Serikali kwa kuwezesha huduma ya upimaji wa udongo kwa kutumia skana, huduma inayotolewa bure kwa wakulima.
Kwa upande wake, Mratibu wa zao la kahawa wilayani Moshi, Magambo Mongera, alisema matumizi ya miche bora chotara yamepunguza gharama za uzalishaji kwa kiasi kikubwa.
Alisema miche hiyo pia inahimili magonjwa na huanza kuzaa mapema, ndani ya miaka miwili na nusu tangu kupandwa.
Aliongeza kuwa mche mmoja unaweza kutoa kati ya kilo tatu hadi tano endapo utatunzwa vizuri.
Mongera alisisitiza umuhimu wa wakulima kutumia teknolojia bora, ikiwemo kupima udongo na kupanda miche chotara, ili kuongeza uzalishaji na kipato.





