WATOTO 127 WAGUNDULIKA NA TB WILAYA YA SIHA

SIHA-KILIMANJARO.

WATOTO 127 wenye umri chini ya miaka 14 waligundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) katika kampeni ya uchunguzi wa afya iliyofanyika mwaka 2025 wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 17 ya wagonjwa wote waliobainika, kiwango kinachozidi wastani wa kimataifa wa asilimia 10 kwa watoto, hali inayotajwa kuwa ya kutia wasiwasi na inayohitaji hatua za haraka.

Hayo yalibainishwa jana na Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Wilaya ya Siha, Dk. Michael Mushi, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Hospitali Maalumu ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH), ambapo alisema hali hiyo inaonesha ukubwa wa tatizo hilo kwa watoto.

Kwa mujibu wa Dk. Mushi alisema wilaya ha Siha ilikuwa na lengo la kugundua wagonjwa 864 wa kifua kikuu, lakini wagonjwa 752 walifanikiwa kubainika, sawa na asilimia 87 ya lengo na kati ya wagonjwa hao, watoto chini ya miaka 14 walikuwa 127.

“Idadi hii ni kubwa na inapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa watoto ni kundi nyeti katika jamii,” alisema.

Dk. Mushi alibainisha kuwa ongezeko la wagonjwa waliogundulika linachangiwa na maboresho ya huduma za afya, ikiwemo kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma na kusogezwa kwa huduma karibu na wananchi.

"Kwa sasa Wilaya ya Siha ina vituo 33 vinavyotoa huduma za afya, hatua ambayo imewezesha wananchi wengi kufanyiwa uchunguzi na kugundulika mapema."alisema.

Alisema kuwa hapo awali upungufu wa vituo vya afya ulisababisha wagonjwa wengi, hususan watoto, kutogundulika mapema, hali iliyochangia kuenea kwa ugonjwa huo kimyakimya.

Aliongeza kuwa kifua kikuu ni ugonjwa unaoambukiza, ambapo mara nyingi watoto huambukizwa kutoka kwa watu wazima wanaoishi nao katika kaya.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH) Dk.Leonard Subi, Afisa Ustawi wa Jamii Wazoeli Mshana alisema hospitali hiyo hupokea zaidi ya wagonjwa 100 wa kifua kikuu kila mwaka, wengi wao wakiwa katika hali mbaya.

Alisema hali hiyo inaonesha bado kuna uhitaji mkubwa wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kupima afya mara kwa mara ili kugundua magonjwa mapema.



Aidha Mshana alisema ili matibabu yaweze kuwa yenye ufanisi zaidi, aliwataka wagonjwa hao kuwa wafuasi wazuri wa dawa hizo.

"Ili matibabu yaweze kuwa yenye ufanisi, mgonjwa wa kifua kikuu aweze kupona na kurejea nyumbani kwake kuendelea na shughuli njia pekee ya kuweza kupona ni kuwa mfuasi mzuri wa dawa, ikiwemo kumeza kwa wakati dawa kwa kuzingatia taratibu na maelekezo wanayopatiwa na wataalamu,"alisema Mshana.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa niaba ya wengine baadhi wagonjwa wa kifua kikuu Mariam Athuman, Zawadi Magimbwala, wanaotibiwa hospitalini hapo waliipongeza serikali kwa kutoa matibabu ya kifua kikuu bila gharama, wakisema hatua hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa watu wengi wasioweza kumudu gharama za matibabu.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.