MIRERANI-SIMANJIRO.
WACHIMBAJI wa madini katika migodi ya Tanzanite iliyopo mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wametakiwa kuacha tabia ya kukimbilia waganga wa kienyeji wanapogundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu, na badala yake kufuata matibabu sahihi ya hospitalini.
Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la Mwitikio wa Kudhibiti Kifua Kikuu na UKIMWI Kanda ya Kaskazini, Thobias Chacha, wakati akizungumzia hali ya magonjwa ya kifua kikuu na silicosis katika maeneo ya migodi ya Mirerani.
Alisema watu wengi wenye viashiria vya ugonjwa huo wamekuwa wakikimbilia tiba za asili, hali inayosababisha kuchelewa kubainika kwa wagonjwa wakati wa kampeni za uchunguzi.
“Watu wengi hasa vijana hujitokeza kupima wakiwa tayari wameathirika zaidi. Wengi wao huja hospitalini wakiwa katika hali mbaya baada ya kujaribu tiba mbadala bila mafanikio.”
Aliongeza kuwa baadhi ya wachimbaji hutumia dawa za miti shamba kama mwarobaini na shubiri, huku wengine wakiamini waganga wa kienyeji wanaodai kuwa wanaweza kuponya ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Chacha, baadhi ya wagonjwa huaminishwa kuchinja mbuzi na kunywa supu yake kama tiba, jambo linalochelewesha kupata matibabu sahihi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wilayani Simanjiro, Daktari Swetbert Patrick, alisema ugonjwa wa silicosis unaosababishwa na kuvuta vumbi la silica migodini huwapata zaidi wachimbaji waliodumu kazini kwa miaka 10 hadi 15.
Alisema pia kuna ongezeko la maambukizi ya kifua kikuu kwa watoto, ambapo wengi huambukizwa na wazazi wao wanaofanya kazi migodini.
“Wachimbaji wanaporudi nyumbani huweza kuwaambukiza watoto wao, na tayari tumeona ongezeko la visa vya watoto wadogo kuugua kifua kikuu.”
Katika jitihada za kudhibiti tatizo hilo, amesema kampeni ya uchunguzi wa kifua kikuu mwaka jana ililenga kubaini wagonjwa 706, lakini waliopatikana ni 416 ambao walianzishiwa matibabu.
Serikali pia imeanza kuchukua hatua kwa kushirikiana na mamlaka za usimamizi wa migodi, kwa kuhakikisha uwepo wa visima na matanki ya maji ili kupunguza vumbi katika maeneo ya uchimbaji.
Baadhi ya vijana wanaougua kifua kikuu Jonas Stanley Makota na Willy Makao, wamesema bado kuna mwamko mdogo wa kupima afya, huku wakitoa wito kwa jamii kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya.
“Nitoe wito kwa vijana wenzangu kubadilika na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu.”alisema Makota.








