SIHA-KILIMANJARO.
HOSPITALI Maalum ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto, iliyopo wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, ilianzishwa mwaka elfu moja mia tisa ishirini na sita na Daktari Nirman Davis, raia wa Uingereza, ikiwa kama kituo cha kuwahudumia wagonjwa wa kifua kikuu pamoja na kufanya tafiti za ugonjwa huo.
Mnamo tarehe ishirini na tisa Oktoba mwaka elfu moja mia tisa hamsini na mbili, kituo hicho kilizinduliwa rasmi na Lady Twining, mke wa aliyekuwa Gavana wa Tanganyika, na kupandishwa hadhi kuwa hospitali maalum ya kifua kikuu, ikihudumia wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kati.
Katika miaka ya sabini, hospitali hiyo ilikuwa miongoni mwa vituo vya kimataifa vya tafiti chini ya taasisi ya Medical Research Council ya Uingereza, ambapo ilichangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa dawa za kutibu kifua kikuu na kusaidia kudhibiti ugonjwa huo duniani.
Hata hivyo, kuibuka kwa virusi vya UKIMWI miaka ya themanini kulisababisha kuongezeka kwa maambukizi ya kifua kikuu, hasa barani Afrika, sambamba na kuibuka kwa aina sugu ya ugonjwa huo inayojulikana kama MDR-TB.
Kutokana na changamoto hiyo, mwaka elfu mbili na nne serikali ilianza kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo pamoja na kuongeza wataalamu ili kukabiliana na kifua kikuu sugu na kupunguza madhara kwa wagonjwa.
Huduma za matibabu ya kifua kikuu sugu zilianza rasmi mwaka elfu mbili na tisa, huku juhudi za kuimarisha hospitali hiyo zikiendelea.
Aidha, mwaka elfu mbili na kumi, Wizara ya Afya ilitangaza kupandisha hadhi hospitali hiyo kupitia Tangazo la Serikali namba mia nane ishirini na nane, na kuifanya kuwa hospitali maalum ya juu ya magonjwa ya kuambukiza.






