MOSHI-KILIMANJARO.
JITIHADA za kuboresha na kuinua kiwango cha elimu katika Kata ya Kiusa zimeendelea kushika kasi, baada ya kufanyika kwa kikao muhimu kilichowakutanisha walimu wa shule za msingi na sekondari katika kata hiyo.
Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Shule ya msingi Muungano, kikilenga kujadili mikakati ya kuboresha taaluma, kuhamasisha uwajibikaji, pamoja na kuwapongeza walimu kwa utendaji wao katika muhula wa kwanza;
Ambapo walimu waliofanya vizuri walitunukiwa zawadi kama sehemu ya motisha ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
Diwani wa Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, aliyasema hayo Machi 27,2016 wakati wa kikao chake na walimu wa shule za msingi na sekondari zilizopo katika kata hiyo, kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya msingi Muungano.
Shekoloa amesema kuwa juhudi za pamoja zinahitajika katika kuinua kiwango cha elimu ndani ya kata hiyo, akisisitiza ushirikiano kati ya walimu, wazazi na viongozi wa serikali za mitaa.
Amesema lengo la kikao hicho ilikuwa ni kujadili mikakati ya kuboresha taaluma, kuhamasisha uwajibikaji pamoja na kuwapongeza walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Aidha, aliwakumbusha wazazi na walezi umuhimu wa kuchangia huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi, akibainisha kuwa suala hilo lina mchango mkubwa katika kuongeza mahudhurio na umakini wa wanafunzi darasani.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuwapa motisha walimu wanaofundisha madarasa ya mitihani, ikiwemo darasa la pili, la nne na la saba kwa shule za msingi, pamoja na kidato cha pili na cha nne kwa upande wa sekondari.
Akizungumza kwa niaba ya walimu, Mkuu wa shule ya msingi Muungano, Athuman Msuya, alisema walimu wamefurahishwa na kikao hicho, akieleza kuwa ni mara ya kwanza kufanyika na kimeongeza ari ya kazi kwa kutambua mchango wao.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule ya sekondari Kiusa, Mariagoreth Maliga, alimpongeza diwani huyo kwa kuandaa ziara za kielimu (outing) kwa walimu kila baada ya miezi sita, hatua aliyosema itasaidia kuongeza uelewa na maarifa, hususan katika masuala ya uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa elimu wa Kata, Msami Kanuti, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote wa elimu ili kufikia matokeo chanya ya kitaaluma.
Naye Afisa mtendaji wa Kata ya Kiusa, Dativa Tesha, aliwahimiza walimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya taaluma yao, huku akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Kikao hicho kimeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika juhudi za kuinua kiwango cha elimu katika Kata ya Kiusa.








