Diwani wa Kata ya Kiusa Khalid Shekoloa, akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Muungano, baada ya kuwakabidhi zawadi zao.
MOSHI-KILIMANJARO.
DIWANI wa Kata ya Kiusa katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Khalid Shekoloa, amewakabidhi zawadi wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yote kwenye mitihani ya robo ya muhula, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ufaulu zaidi shuleni.
Akizungumza Machi 27, 2026 wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi hizo, Shekoloa alisema lengo la zoezi hilo ni kuongeza ari ya kujifunza kwa wanafunzi wa shule za msingi Jamhuri, Muungano pamoja na shule ya sekondari Kiusa.
Zawadi zilizotolewa ni pamoja na mabegi, madaftari, kompasi na fedha taslimu kwa wanafunzi watatu bora kutoka darasa la kwanza hadi la saba.
Kwa upande wa shule ya sekondari Kiusa, wanafunzi waliofanya vizuri pia walipatiwa zawadi mbalimbali zilizolenga kuwapa motisha ya kuendelea kufanya vizuri zaidi kitaaluma.
Aidha, Shekoloa aliwapongeza walimu kwa juhudi wanazozifanya katika kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika masomo yao, akisisitiza kuwa mafanikio ya wanafunzi yanatokana na ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe.
Alisema zawadi hizo ni sehemu ya kutia motisha kwa wanafunzi ili waendelee kuongeza bidii katika masomo yao, huku akiwataka kujiepusha na makundi mabaya yanayoweza kuharibu ndoto zao za baadaye.
“Jitahidini kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu ili muweze kufikia malengo yenu ya maisha,” alisisitiza Shekoloa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kiusa, Mariagoreth Malinga, alimshukuru diwani huyo kwa mchango wake katika kuinua elimu, akieleza kuwa hatua hiyo itawapa hamasa kubwa wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yao.
Naye Mkuu wa Shule ya msingi Jamhuri, Salome Ngoti, pamoja na Mkuu wa Shule ya msingi Muungano, Athuman Msuya, kwa pamoja walitoa shukrani zao kwa diwani Shekoloa wakisema kuwa zawadi hizo zimekuwa chachu ya mafanikio kwa wanafunzi na zitachangia kuboresha kiwango cha taaluma katika shule hizo.
Waliongeza kuwa ushirikiano huo kati ya viongozi na shule ni muhimu katika kukuza elimu na kuwajengea wanafunzi mazingira bora ya kujifunza.









