MOSHI-KILIMANJARO.
WADAU wa michezo, hususan soka, mkoani Kilimanjaro wamempongeza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Injiniya Zuberi Abdallah Kidumo, kwa juhudi zake za kuendeleza miundombinu ya michezo kupitia ukarabati wa uwanja wa Nelson Mandela uliopo Kata ya Bomambuzi.
Pongezi hizo zilitolewa Machi 25, 2026 na Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), Abdallah Thabit, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea uwanja huo.
Amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya uongozi wa Manispaa katika kukuza vipaji vya vijana kupitia michezo.
“Kama wadau wa michezo, tunajivunia kuona kiongozi anayetekeleza ahadi kwa vitendo, alianza na uwanja wa Railway-Njoro na sasa ameanza ukarabati wa uwanja wa Nelson Mandela,” amesema Thabit.
Ameongeza kuwa maendeleo ya soka yanategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa miundombinu ya viwanja, akisisitiza kuwa viwanja vibovu vinakwamisha juhudi za kuinua vipaji vya vijana.
“Ni vigumu kupata wachezaji bora kama viwanja ni duni, tunampongeza sana Meya Kidumo kwa jitihada zake hizi za kuboresha viwanja ndani ya Manispaa ya Moshi,” amesisitiza.
Thabit pia amebainisha kuwa ujenzi na ukarabati wa viwanja unahitaji rasilimali kubwa za kifedha, na kuwataka wadau wengine kujitokeza kumuunga mkono meya huyo ili kufanikisha azma hiyo.
Kwa upande wake, mdau wa soka Pascal Muhera amesema kuwa kwa mujibu wa sheria za mpira wa miguu za FIFA, uwanja bora ni msingi muhimu wa mchezo huo.
Ameeleza kuwa kwa muda mrefu wakazi wa Moshi wamekuwa wakilalamikia ubovu wa viwanja, hali iliyokuwa inarudisha nyuma maendeleo ya soka.
Muhera ameongeza kuwa Meya Kidumo ameonesha dhamira ya kweli ya kubadilisha hali hiyo kwa kuanza na uwanja wa Railway-Njoro na sasa kuendelea na uwanja wa Nelson Mandela, hatua ambayo inapaswa kuungwa mkono na jamii nzima.
Akizungumzia juhudi hizo, Meya Injia Zuberi Abdallah Kidumo amesema uwekezaji katika michezo ni sehemu ya mkakati wake wa kukuza afya, nidhamu, ajira na mshikamano miongoni mwa wakazi wa Manispaa ya Moshi.
Alikumbusha kuwa mwaka 2025, wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Zuberi Cup, aliahidi kuendeleza ukarabati wa viwanja vya michezo baada ya mafanikio ya uwanja wa Railway-Njoro, akielekeza nguvu kwenye uwanja wa Nelson Mandela uliopo Bomambuzi.
"Lengo langu ni kuhakikisha kila kata ndani ya Manispaa inakuwa na uwanja wa michezo unaokidhi mahitaji ya jamii."amesema.
Aidha, Meya Kidumo ameeleza azma yake ya kuendeleza michezo kwa soka la wanawake kwa kujenga uwanja maalum wa netiboli, ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika michezo na mashindano mbalimbali.





