MOROGORO-TANZANIA.
MAMLAKA Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) imeendelea kuonesha ubora wake katika utoaji wa huduma kwa wananchi baada ya kunyakua tuzo mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Katika mwaka wa fedha 2024/25, MUWSA imeibuka mshindi wa kwanza katika utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira, katika kundi la mamlaka zinazohudumia zaidi ya wateja elfu 20.
Ushindi huo unaifanya mamlaka hiyo kuendeleza rekodi yake ya kufanya vizuri mfululizo katika sekta hiyo muhimu.
Tuzo hizo hutolewa kama chachu ya kuimarisha utawala bora na kuongeza uwajibikaji kwa watoa huduma, huku zikilenga kuhakikisha malengo ya Serikali na matarajio ya wananchi yanafikiwa kwa viwango vya juu, hasa katika huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
Kupitia mafanikio hayo, MUWSA imeendelea kujipambanua kama moja ya mamlaka zinazotoa huduma bora na zenye kuzingatia mahitaji ya wananchi.




