MATIBABU YA KIFUA KIKUU YABORESHWA, MUDA WAPUNGUZWA HADI MIEZI SITA

 


SIHA-KILIMANJARO.

MATIBABU ya wagonjwa wa kifua kikuu, hususan kifua kikuu sugu (TB sugu), yameendelea kuboreshwa nchini kufuatia kupungua kwa muda wa tiba kutoka miaka miwili hadi miezi sita, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa tiba na kupunguza madhara kwa wagonjwa.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Kifua Kikuu Sugu katika Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH), Dk. Happiness Mvungi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani.

Dk. Mvungi alisema hapo awali matibabu ya kifua kikuu sugu yalikuwa yakichukua kati ya miezi 18 hadi 20, yakihusisha matumizi ya sindano na vidonge. Hata hivyo, mabadiliko ya miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) yamewezesha kuondolewa kwa sindano na kubaki na tiba ya vidonge pekee.

Alifafanua kuwa matumizi ya sindano yalikuwa na changamoto kubwa kwa wagonjwa, ikiwemo madhara ya kupoteza uwezo wa kusikia na matatizo ya figo, hali iliyochangia kuboreshwa kwa tiba hizo.

“Kuanzia mwaka 2019 wagonjwa walianza kutumia vidonge pekee, na mwaka 2020 muda wa matibabu ukapunguzwa hadi miezi tisa hadi 11. Mwaka 2022, WHO ilitoa mwongozo mpya wa kupunguza zaidi muda huo hadi miezi sita,” alisema Dk. Mvungi.

Aliongeza kuwa Tanzania imeanza kutekeleza matibabu hayo ya muda mfupi, ambapo mgonjwa hutumia dawa nne tu kwa kipindi cha miezi sita, tofauti na awali ambapo alitumia dawa sita hadi saba kwa muda mrefu zaidi.

Kwa mujibu wa Dk. Mvungi, mafanikio ya matibabu hayo ni makubwa, ambapo asilimia 75 ya wagonjwa wamepona, ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa asilimia 63.

Hata hivyo, alibainisha kuwa tafiti zinaendelea kufanyika ili kuona uwezekano wa kupunguza zaidi muda wa matibabu.

Kwa upande wake, Daktari Marco Adam Janga kutoka wodi ya kifua kikuu alisema wagonjwa wa kifua kikuu cha kawaida hutibiwa kwa miezi sita, ambapo katika miezi miwili ya mwanzo hutumia dawa mchanganyiko wa aina nne, kisha kuendelea na dawa mbili kwa kipindi kinachofuata.

Alisema baada ya kukamilisha matibabu, mgonjwa hupimwa makohozi ili kufuatilia maendeleo ya afya yake.

Naye Afisa Muuguzi katika wodi ya wagonjwa wa kifua kikuu sugu, Winfrida Manyaza, alisisitiza umuhimu wa ufuasi sahihi wa matumizi ya dawa kwa wagonjwa, akieleza kuwa kutofuata maelekezo kunaweza kusababisha kuongezeka kwa usugu wa ugonjwa.

“Ufuasi mzuri wa dawa husaidia kuua vimelea na kusafisha makohozi. Mgonjwa asipotumia dawa ipasavyo, anaweza kupata kifua kikuu sugu zaidi,” alisema.

Kwa upande mwingine, Afisa Ustawi wa Jamii, Sylivester Madirisha, alisema hospitalini humo kuna programu maalum za mazoezi na michezo kwa wagonjwa wanaokaa muda mrefu wodini, lengo likiwa ni kuimarisha afya ya akili na kuwasaidia kuhimili matibabu yao.

Alisema mazoezi hayo huchangia kuwajenga wagonjwa kisaikolojia na kuwapa nguvu ya kuendelea na tiba hadi kupona.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.