SIHA-KILIMANJARO.
JAMII imetakiwa kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kwa kutambua dalili zake mapema na kuchukua hatua stahiki ili kujikinga na maambukizi yanayoweza kuepukika.
Hayo yalisemwa Machi 19,2026 na Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH), Dk. Leonard Subi, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 24.
Alisema kifua kikuu ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na bakteria na husambaa kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Dk. Subi alisema ugonjwa huo unaweza kuwa hatari zaidi endapo hautagundulika mapema, na kuongeza kuwa dalili zake kuu ni pamoja na kukohoa kwa zaidi ya wiki mbili, kupoteza uzito bila sababu, homa za mara kwa mara hasa nyakati za jioni, pamoja na jasho jingi wakati wa usiku.
Alisema kuwa uwepo wa mtu mwenye maambukizi ya kifua kikuu katika mazingira ya nyumbani au kazini huongeza hatari ya kuambukizwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa afya, ikiwemo kupima mara kwa mara na kuboresha mazingira ya makazi na sehemu za kazi.
Aidha, alifafanua kuwa kifua kikuu kinatibika hasa kinapogundulika mapema, akitaja kuwepo kwa aina ya kawaida inayotibiwa kwa dawa za mstari wa kwanza na ile sugu inayohitaji dawa maalum za mstari wa pili pamoja na uangalizi wa kitaalamu wa karibu zaidi.
Kwa upande wa huduma, Dk. Subi alisema Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto, imeendelea kuwa kituo cha mfano katika utoaji wa matibabu ya kifua kikuu, ikiwemo kwa wagonjwa wa TB sugu, ambapo huduma hutolewa kwa gharama za Serikali ili kuhakikisha kila mgonjwa anapata matibabu stahiki.
