MOSHI-KILIMANJARO.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, ametangaza kusudio lake la kuwasilisha bungeni hoja binafsi itakayolenga kuishauri Serikali kuleta marekebisho ya sheria za vyama vya ushirika ili kuimarisha uwajibikaji na kulinda fedha za wakulima.
Makoi alitoa kauli hiyo wakati akisalimu katika hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa miche bora ya kahawa uliofanyika katika kijiji cha Kiruweni, kata ya Mwika Kusini, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Alisema sheria zilizopo za vyama vya ushirika bado zina mapungufu makubwa, ikiwemo kushindwa kuwabana ipasavyo viongozi wanaojihusisha na ubadhirifu wa fedha za wakulima katika vyama vya msingi.
“Ni muhimu sheria hizi zibadilishwe ili ziwe na makali ya kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kutafuna fedha za wakulima,” alisema Makoi.
Alieleza kuwa baadhi ya viongozi waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia vyama vya ushirika wamekuwa si waaminifu, licha ya wakulima kuweka fedha zao kama akiba kwa ajili ya kuendeleza zao la kahawa katika misimu inayofuata.
Katika hatua nyingine, Makoi alimkumbuka aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, marehemu Augustino Lyatonga Mrema, kwa mchango wake mkubwa katika kusimamia na kufufua zao la kahawa.
Alisema licha ya wakulima wengi kuachana na kilimo cha kahawa kwa zaidi ya miaka 15 kutokana na kukosa tija, juhudi za Mrema ziliwezesha kurejea kwa kilimo hicho ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa wakazi wa Kilimanjaro.
“Hakika hatutamsahau Mrema kwa kazi kubwa aliyoifanya katika maeneo ya Vunjo na Moshi Vijijini,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola, alisema wamejipanga kuhakikisha wanafufua zao la kahawa kwa vitendo.
Alisema majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini yamekusudia kugawa jumla ya miche bora ya kahawa milioni moja, ambapo kila jimbo litapata miche 500,000 kwa ajili ya wakulima.
Koola aliwataka vijana kujikita katika kilimo cha kahawa akibainisha kuwa bei ya zao hilo imeendelea kuimarika kwa sasa, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.


















