KAHAWA NI DHAHABU YA KIJANI, MOSHI VIJIJINI KUNUFAIKA NA MICHE 267,000

MOSHI-KILIMANJARO.

KATIKA jitihada za kufufua zao la kahawa na kuongeza kipato kwa wakulima, jumla ya miche bora chotara ya kahawa 267,000 inatarajiwa kugawiwa kwa wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.

Miche hiyo ambayo imetolewa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uzalishaji wa zao la kahawa nchini na kurejesha hadhi yake kama zao muhimu la biashara kwa wakulima wa maeneo ya ukanda wa milimani.

Uzinduzi wa ugawaji huo unatarajiwa kufanyika Aprili 8,2026 katika Kijiji cha Kishimundu, kilichopo Kata ya Uru Mashariki, Wilayani Moshi Vijijini mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, akizindua rasmi zoezi hilo litakalowahusisha wakulima kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, amesema ugawaji wa miche hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa wakati wa kampeni, akilenga kufufua kilimo cha kahawa ambacho kimekuwa kikidorora katika miaka ya hivi karibuni.

Makoi amesema kati ya kata 16 zilizopo jimboni humo, kata 14 zilizoko katika ukanda wa milimani zinafaa kwa kilimo cha kahawa, hivyo kuna fursa kubwa kwa wananchi kuongeza uzalishaji na kipato kupitia zao hilo.

Uzinduzi huo utakwenda sambamba na Kauli Mbiu isemayo, “Kahawa Ni Dhahabu ya Kijani, Twende Tukailime,” ikiwa ni wito kwa wakulima kurejea kwa wingi katika kilimo cha kahawa na kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na zao hilo.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu.


Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava.

Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Morris Makoi.

Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) PRIMUS KIMARYO.


Mbunge wa Jimbo la Vunjo Mhe; Enock Zadock Koola.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.