MOSHI-KILIMANJARO.
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi (MMC) mkoani Kilimanjaro wameidhinisha bajeti ya jumla ya Sh bilioni 58.7 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayotarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na miundombinu katika Manispaa hiyo.
Akitoa taarifa hiyo Februari 14,2026, Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo, Zuberi Kidumo, alisema bajeti hiyo inajumuisha Sh bilioni 12.3 zitakazotokana na vyanzo vya mapato ya ndani, ikilinganishwa na makadirio ya Sh bilioni 11.3 yaliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi (MMC), Mwajuma Nasombe, alisema katika mwaka wa fedha 2026/2027 halmashauri imetenga Sh bilioni 1.4 kwa ajili ya sekta ya elimu, fedha zitakazotokana na mapato ya ndani.
“Fedha hizi zimetengwa kwa mujibu wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayotaka halmashauri kutumia mapato yao ya ndani kuboresha sekta ya elimu.
Miongoni mwa matumizi yake ni ujenzi wa madarasa mapya kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari mwaka 2028,” alisema.
Alifafanua kuwa Manispaa inatarajia kuwa na wanafunzi 9,241 watakaojiunga na elimu ya sekondari mwaka 2028, hali inayohitaji ujenzi wa jumla ya madarasa 185 mapya ili kukidhi mahitaji hayo.
Nasombe alisema baraza linaendelea na mikakati ya kufunga taa za barabarani pamoja na taa za kuongozea magari katika maeneo mbalimbali ya mji wa Moshi, kwa lengo la kuimarisha usalama na kurahisisha usafiri nyakati za usiku.
Aidha, alieleza kuwa kuna mpango wa kuboresha barabara ya Kibo kuanzia Mnara wa Saa katikati ya mji wa Moshi hadi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC kupitia barabara ya Sokoine.
"Mradi huo utatekelezwa kwa awamu na unalenga kuipanua barabara hiyo kuwa ya njia nne kutokana na umuhimu wake wa kiuchumi na kijamii."alisema.
Alibainisha kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu kinachoelekea Hospitali ya Rufaa ya KCMC, taasisi zaidi ya tano za elimu ya juu pamoja na kuelekea eneo la Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Mweka, Kibosho.
Pia Mkurugenzi huyo alitoa rai kwa madiwani kuendelea kushirikiana na Wataalamu wa Manispaa ili kuhakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Kwa upande wake, Mbunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, alielezea kuridhishwa kwake na bajeti hiyo, akisema itasaidia kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikikabili wananchi kwa muda mrefu.
“Baadhi ya changamoto hizo ni ukosefu wa taa za barabarani, huduma duni za ukusanyaji taka na ubovu wa miundombinu ya barabara, kwa ushirikiano mzuri, tupo katika nafasi ya kutekeleza ahadi tulizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi,” alisema.
Bajeti hiyo inatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya mji wa Moshi kwa kuimarisha sekta za elimu, miundombinu na huduma za kijamii kwa ujumla.













