UWT MOSHI MJINI, YAPONGEZA MAFANIKIO YA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA

MOSHI-KILIMANJARO.

UMOJA wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Moshi Mjini umempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa mafanikio ya siku 100 madarakani, yakihusisha utoaji wa ajira katika sekta za elimu na afya pamoja na kuimarishwa kwa mikopo kwa makundi maalumu.

Pongezi hizo zimetolewa Februari 14, 2026 na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Moshi Mjini, Teddy Komba, wakati wa ufunguzi wa kikao cha kawaida cha Baraza la UWT kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, mjini Moshi.

Teddy, amesema Rais Samia ameendelea kubeba ajenda ya kumuinua mwanamke, vijana na makundi maalumu kwa kuweka mazingira rafiki ya kiuchumi na kijamii, hatua inayochochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Amesema katika kikao hicho, wajumbe wanatarajia kujadili masuala ya haki na usawa wa wanawake pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ambapo mada itawasilishwa na Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Kilimanjaro.

Aidha, Komba amesema UWT inaendelea kuwajengea uwezo wanawake kushika nafasi mbalimbali za uongozi, huku akiwapongeza madiwani wanaotokana na jumuiya hiyo, kwa kuonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi na uwakilishi ndani ya baraza la madiwani.

Akizungumzia uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi, Teddy amesisitiza umuhimu wa mikopo inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalumu, akiiomba serikali kuhakikisha fedha za Rais Samia shilingi milioni 200 zilizotengwa kwa ajili ya wajasiriamali zinawafikia walengwa.

“Wengi wa akina mama wanajishughulisha na biashara za ujasiriamali, hivyo tunaomba fedha hizo ziweze kuwafikia kwa wakati ili ziendelee kuwainua kiuchumi,” amesema Komba.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.