MOSHI-KILIMANJARO.
TIMU ya Hai United imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Zuberi Cup baada ya kuichapa Fire FC mabao 2-0 katika mchezo wa robo fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Railway Njoro, Moshi.
Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkali, huku kila timu ikisaka ushindi ili kusonga mbele katika mashindano hayo.
Kipindi cha kwanza timu hizo zilitoshana nguvu, zikishambuliana kwa zamu, lakini hadi dakika 45 hakuna iliyoweza kupata bao.
Kipindi cha pili, Hai United ilirejea ikiwa na kasi zaidi na kupata bao la kwanza kupitia kwa Waziri Issa, kabla ya Joachim Saimon kuongeza bao la pili na kuifanya timu hiyo kuwa mbele kwa mabao 2-0 hadi mwisho wa mchezo.
Katika dakika za mwisho za mchezo huo, mlinda mlango wa Fire FC, Joseph Semsei, alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kwenda kumsukuma mwamuzi wa kati kufuatia kutoridhishwa na uamuzi wa kulikubali bao la pili la Hai United, hatua hiyo iliifanya Fire FC kumaliza mchezo ikiwa pungufu.
Akizungumza baada ya mchezo, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Hassan Bomboko, ameipongeza Hai United kwa kupata ushindi huo, akisema timu hiyo imepata matokeo iliyostahili kutokana na juhudi ilizozionyesha uwanjani.
Aidha, amewapongeza waandaaji, waratibu pamoja na mdhamini wa mashindano hayo, Zuberi Abdallah Kidumo, kwa kufanikisha mashindano yanayowakutanisha wananchi kwa wingi.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Hai United, Shaban Msango, amewapongeza wachezaji wake kwa kutekeleza maelekezo aliyowapa kabla na wakati wa mchezo.
Amesema mpango wake ulikuwa kuhakikisha timu inapata matokeo mapema, akieleza kuwa walitambua mpinzani wao alikuwa amejiandaa kwa ushindani mkubwa.
Naye Kocha wa Fire FC, David John, ameipongeza Hai United kwa ushindi huo, akisema wapinzani wao walijiandaa vizuri na kufanikiwa kutumia maeneo ambayo Fire FC ilikuwa na udhaifu.
Amesema Fire FC sasa itaweka nguvu katika maandalizi ya mashindano yajayo ya Zuberi Cup mwakani.
![]() |
![]() |



















