WAZIRI MKUU DK. MWIGULU NCHEMBA, ATOA ONYO KALI KWA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WAZEMBE

NDUNGU-SAME.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu  Lameck Nchemba, amesema serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya Wakurugenzi wa halmashauri nchini wanaoshindwa kusimamia ipasavyo fedha za miradi ya maendeleo.

Amesema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wakurugenzi kupokea fedha kutoka serikalini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, lakini badala yake kuzichepusha au kuzitumia visivyo, huku wananchi wakiendelea kukosa huduma muhimu za afya, maji na elimu.

“Haya mambo ya fedha kuletwa halafu zinakaliwa, zinachepushwa na watu kulipana posho wakati wananchi wanateseka, hatukubaliani nayo,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Ndungu, Jimbo la Same Mashariki, Wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Katika ziara hiyo, Dk. Nchemba alitaka maelezo ya kina kuhusu fedha zilizotolewa mwaka jana kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Suji–Gonjaza, ambazo hadi sasa hazijaanza kutumika kwa ujenzi huo, licha ya wananchi kuhitaji huduma za afya kwa haraka.

Aidha, alihoji matumizi ya shilingi milioni 248 zilizotolewa katika eneo la Hedaru kwa ajili ya ujenzi wa madarasa saba, ambapo madarasa manne pekee ndiyo yaliyojengwa, huku fedha za madarasa matatu zikidaiwa kutojulikana zilipoelekezwa.

Waziri Mkuu pia alieleza kusikitishwa na hali ya majengo katika Hospitali mpya ya Wilaya ya Same, ambayo tayari yanaonekana kuwa na nyufa licha ya kuwa mapya. Vilevile, aligusia ujenzi wa madarasa saba katika eneo la Kihurio ambayo yalianguka ndani ya kipindi cha miaka mitatu tangu yajengwe.

Kutokana na tuhuma hizo, Waziri Mkuu alimuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro kufanya uchunguzi wa kina katika maeneo yote yaliyotajwa na kuwasilisha taarifa kabla ya kumaliza ziara yake mkoani humo.

Sambamba na hilo, alimwagiza Waziri wa TAMISEMI kufuatilia kwa karibu tuhuma hizo na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa iwapo itabainika kulikuwa na uzembe au ubadhirifu wa fedha za umma.

“Tutakapobaini uzembe au ubadhirifu, wahusika watachukuliwa hatua kali bila kusita,” alisisitiza


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.