MWANGA-KILIMANJARO.
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amewataka watumishi wa umma kuongeza kasi na ufanisi katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati inayotekelezwa katika maeneo yao ya kazi, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.
Waziri Mkuu alitoa wito huo wilayani Mwanga wakati wa uzinduzi wa hospitali mpya ya wilaya iliyogharimu shilingi bilioni 2.9, akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kuboresha huduma za kijamii na miundombinu ya maendeleo nchini.
Alisema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Samia Suluhu Hassan, Serikali imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya kwa kujenga hospitali katika kila wilaya ambayo hapo awali haikuwa na hospitali.
Aidha alisema katika kipindi hicho serikali imejenga vituo vya afya 649 na zahanati 2,800 zimejengwa ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Katika sekta ya elimu, Waziri Mkuu alisema Serikali imejenga shule za sekondari 1,300 nchi nzima, shule za msingi 2,700 pamoja na madarasa 79,000, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mwanga, Dk. Ngwaru Maghembe, alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, zaidi ya shilingi bilioni 60 zimeletwa jimboni humo kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Alifafanua kuwa katika sekta ya afya pekee, jimbo hilo limepokea zaidi ya shilingi bilioni 8, huku sekta ya elimu ikipewa shilingi bilioni 8.6 na shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa shule tatu za sekondari na shule tatu za msingi.
Aidha, katika sekta ya Nishati, Serikali ilitoa shilingi bilioni 8.7 kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambapo vijiji vyote katika jimbo hilo tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme.
Mbunge huyo aliongeza kuwa katika bajeti inayoendelea, Serikali imetoa shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya watoto, wodi ya wazazi (baba) pamoja na jengo la upasuaji, hatua itakayoongeza ubora wa huduma za afya kwa wananchi wa Mwanga na maeneo jirani.

