KIGONIGONI-MWANGA.
NAIBU Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ngwaru Maghembe, ameonesha masikitiko yake kufuatia kusuasua kwa utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji wa Butu–Usangi–Kigonigoni unaotekelezwa na mkandarasi Nolspan International Co. Limited kwa ubia na Elite Co. Limited, wenye thamani ya Sh bilioni 16.8.
Dk. Maghembe, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Kigonigoni katika ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi jimboni humo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Mkazi, Allan Mseppa, alisema hadi sasa mradi umefikia asilimia 8.2 tu ya utekelezaji, wakati ulipaswa kuwa umefikia angalau asilimia 50 kwa mujibu wa ratiba ya kazi.
Akizungumzia hali hiyo, Dk. Maghembe alisema hajaridhishwa na kasi ya mkandarasi na kuahidi kuchukua hatua za haraka kuhakikisha mradi unaenda kwa kasi iliyopangwa.
“Si jambo la kawaida mkandarasi kuwa amefikia asilimia 8.2 pekee wakati muda uliotumika ni nusu ya muda wa utekelezaji. Nitakwenda kuonana na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mhandisi Mndolwa, ili tuweze kumsukuma mkandarasi huyu kuongeza kasi ya ujenzi,” alisema Dk. Maghembe.
Aliongeza kuwa Serikali imetoa fedha hizo kwa lengo la kuwakomboa wakulima wa eneo hilo na kuongeza uzalishaji wa mazao, hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo muhimu.
Aidha, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha Sh bilioni 16.8 kwa ajili ya ujenzi wa skimu hiyo ya umwagiliaji, akibainisha kuwa mradi huo utachochea ongezeko la uzalishaji wa chakula na kuinua kipato cha wananchi wa Wilaya ya Mwanga.
Kwa upande wake, Mhandisi Mseppa alisema mradi huo utakapokamilika utanufaisha wakulima na wadau wa kilimo wapatao 24,000.
Alifafanua kuwa bonde hilo lina uwezo wa kulima hekta 5,000, huku mradi ukiwa na lengo la kuendeleza hekta 800 kwa mfumo wa umwagiliaji wa kisasa, kutoka hekta 300 zilizokuwa zikitumika awali kwa njia za asili.
Alisema mradi huo ni wa siku 540 tangu mkandarasi apewe kazi, na hadi sasa siku 270 zimekwishatumika, hali inayoongeza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia malengo yaliyowekwa, mradi huo ulianza Mei 2025 na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.
Diwani wa Kata ya Kigonigoni, Jeremia Shayo, aliishukuru Serikali kwa kuidhinisha zaidi ya Sh bilioni 16.8 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa umwagiliaji, akisema utakapokamilika utawanufaisha moja kwa moja wakulima zaidi ya 24,000 kutoka Tarafa ya Jipendea.
Naye mkazi wa Butu, Nguluma Kajoto, alisema kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na kuingia katika kilimo cha kisasa chenye tija na manufaa makubwa kiuchumi.
Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji Kigonigoni ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wakulima katika maeneo yenye ukame.












