WAZIRI MKUU DK. MWIGULU NCHEMBA, AWEWATAKA WANAFUNZI KUSOMA.KWA BIDII KUMUUNGA MKONO RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

GARARAGUA-SIHA.

WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amewataka wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Kilimanjaro kusoma kwa bidii ili kuwaenzi wazazi wao sanjari na kuunga mkono jitihada za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Waziri Mkuu Dk. Nchemba aliyasema hayo Februari 21,2026 Wilayani Siha, wakati akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi ioiyoko katika kijiji cha Mawasiliano, Kata ya Gararagua.

Dk. Nchemba alisema juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu zinapaswa kuendana na bidii ya wanafunzi darasani.

“Wanangu someni kwa bidii , kitu pekee cha kuwalipa wazazi wenu na furaha mtakayompa Rais Samia Suluhu Hassan ni kufaulu vizuri katika masomo yenu,” alisisitiza.

Aidha Waziri Mkuu, alifurahishwa na taarifa iliyosomwa mbele yake.kuwa shule hiyo ni ya masomo ya sayansi yenye tahsusi ya PCM (Physics, Chemistry na Mathematics), akiwahimiza wanafunzi kujikita zaidi katika masomo hayo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

“Nilipofika hapa Kilimanjaro Girls’ nilifurahi kusikia kwamba ni shule ya masomo ya sayansi tena ina tahsusi ya PCM, hii imenifanya nikumbuke pure mathematics inayoanza na quadratics, inakuja functions, coordinate geometry na tunamaliza na calculus – differentiation and integration,” alisema huku akishangiliwa na wanafunzi.

Aliwahimiza wanafunzi kuhakikisha wanatumia fursa hiyo vyema kwa kufanya bidii ili wafike vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu.

“Mwanafunzi soma kwa bidii, usiruhusu kufika level hii halafu ukakosa kwenda chuo kikuu au chuo kingine cha elimu ya juu, Rais Dk. Samia amewapa elimu watoto wa Kitanzania kwa kuwatengenezea urithi wa aina hii,” alisema Waziri Mkuu Nchemba.

Kwa mujibu wa taarifa ya ujenzi iliyosomwa mbele ya Waziri Mkuu, jumla ya shilingi bilioni 4.45 zimepokelewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule hiyo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.