KIBONG'OTO SIHA SIHA.
WAZIRI Mkuu, Mwigulu Nchemba, ameipongeza Bodi na Menejimenti ya Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH) kwa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo ya kimkakati inayotekelezwa hospitalini hapo, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la utawala.
Waziri Mkuu alitoa pongezi hizo jana wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo la utawala katika Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong'oto, yenye makao makuu katika Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.
“Nakupongeza Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto pamoja na Menejimenti yako kwa kusimamia vizuri miradi hii ya maendeleo inayotekelezwa hospitalini hapa, ikiwemo ujenzi unaoendelea wa jengo la utawala,” alisema Waziri Mkuu.
Aliongeza kuwa amefika hospitalini hapo kwa kujiamini kutokana na taarifa alizopokea kuhusu utekelezaji mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Nitumie fursa hii pia kuipongeza Bodi ya Hospitali ya Kibong’oto na Menejimenti yote chini ya uongozi wa Mkurugenzi, Dk. Leonard Subi, kwa kazi nzuri wanayoifanya,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutafuta na kutoa fedha nyingi za maendeleo ambazo zimeiwezesha Hospitali ya Kibong’oto kufikia hadhi ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuwa na maabara yenye ithibati ya kimataifa.
Hata hivyo, alitoa onyo kwa baadhi ya wasimamizi wa miradi ya umma wanaokwenda kinyume na matarajio ya Serikali.
“Rais anajitahidi sana kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo, lakini wapo baadhi ya waliokabidhiwa jukumu la kusimamia miradi hiyo ni wazembe. Hatuwezi na hatutawavumilia hata kidogo,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka viongozi wa taasisi na wasimamizi wa miradi ya Serikali kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma.
Akitoa taarifa ya mradi wa ukarabati na upanuzi wa jengo la utawala, Mkurugenzi Mtendaji wa KIDH, Dk. Leonard Subi, alisema kuwa jengo hilo linatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 3.7 hadi kukamilika kwake.
Alifafanua kuwa mradi huo pia unahusisha ujenzi wa nyumba ya walinzi, geti na uzio (fensi) kwa gharama ya shilingi milioni 323.097, pamoja na maegesho ya magari yatakayogharimu shilingi milioni 65.5.
Kwa mujibu wa Dk. Subi, hadi sasa hospitali imepokea shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1.8 tayari zimetumika.
Alieleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa kwa kuimarisha mazingira ya utoaji huduma na kuongeza tija ya watumishi.
“Kukamilika kwa jengo hili kutaiweka taasisi na nchi katika ramani ya kimataifa, kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya na kuimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi,” alisema Dk. Subi.







