MOSHI-KILIMANJARO.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Nchini (TFRA) imewaonya vikali Mawakala wa kusambaza mbolea ya ruzuku watakaobainika kuchezea mfumo huo au kuuza mbolea nje ya utaratibu uliowekwa, ikiahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Onyo hilo limetolewa na Meneja wa TFRA Kanda ya Kaskazini, Gothard Liampawe, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi kuhusu hali ya upatikanaji wa mbolea katika kanda hiyo.
Liampawe alisema wako baadhi ya mawakala wasio waaminifu wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu kwa kuchezea mfumo wa ruzuku, hali inayosababisha taharuki miongoni mwa wakulima.
Alisisitiza kuwa mawakala wote watakaobainika kufanya udanganyifu huo, ikiwa ni pamoja na kuuza mbolea nje ya mfumo wa ruzuku, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungiwa akaunti zao.
“Wapo baadhi ya mawakala ambao si waaminifu, wanauza mbolea nje ya mfumo wa ruzuku, tunawaonya waache mara moja, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Liampawe.
Aliongeza kuwa TFRA inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa wakati, huku mawakala wakitakiwa kuagiza mbolea kulingana na mahitaji yaliyopo.
Aidha, alibainisha kuwa wakati mwingine baadhi ya mawakala hutoa taarifa zisizo sahihi kwa kudai kuwa hakuna mbolea, ilhali hawajafanya malipo kwa kampuni husika, jambo linalochangia kuleta hofu isiyo na msingi kwa wakulima.
Alisema kuna tani 247.5 za mbolea ya kukuzia ambazo mawakala wameshafanyia malipo zimeanza kusafirishwakuletwa mkoani Kilimanjaro hususani kwa wakulima wa Moshi, Hai na Siha.
“Niwahakikishia wakulima kuwa mbolea zipo zinapatikana licha ya ongezeko la uhitaji wa mbolea ya kukuzia kwa sasa katika baadhi ya wilaya za mkoa wa ikiwemo wilaya ya Siha, Hai na Moshi, hivyo wakulima wasibabaishwe na taarifa zinazosambazwa ambazo zinalenga kuleta taharuki na hofu kwa wakukima kwamba mbolea hakuna,"alisema.
Pia alieleza kuwa TFRA imeendelea kuweka kambi Kanda ya Kaskazini ili kuhakikisha upatikanaji wa mbolea unaendelea kuongozeke katika mkoa wa Kilimanjaro hususani Wilaya ya Siha, Moshi na Hai
Kwa upande mwingine, Liampawe alisema serikali imeendelea kuimarisha sekta ya kilimo kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea ulioanza mwaka 2022/2023, hatua inayolenga kuongeza tija kwa wakulima.
Akizungumzia takwimu za wanufaika, alisema hadi sasa jumla ya wakulima 677,808 wamesajiliwa kwenye mfumo wa ruzuku katika Kanda ya Kaskazini, ambapo kati yao wakulima 330,705 tayari wameshanufaika na mpango huo tangu kuanzishwa kwake.
Alisisitiza kuwa TFRA itaendelea kusimamia kwa karibu upatikanaji na ubora wa mbolea ili kuhakikisha wakulima wananufaika kikamilifu na mpango huo wa serikali.













