MOSHI-KILIMANJARO.
MKUU wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, ameibua matumaini ya kupatikana suluhu ya kudumu katika mgogoro wa muda mrefu wa matumizi ya eneo la hifadhi ya barabara (road reserve) uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 kati ya wakazi wa Barabara ya Sukari, mtaa wa Matindigani, na mfanyabiashara Denis Somi.
Mgogoro huo ulitokana na matumizi ya eneo hilo la hifadhi ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitumika na wananchi, hasa vijana, kwa shughuli ndogondogo za ujasiriamali ikiwemo biashara ya kahawa.
Hata hivyo, hivi karibuni mfanyabiashara huyo alidai kukodishiwa eneo hilo kisheria kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vya ujenzi.
Akizungumza wakati wa kusikiliza pande zote za mgogoro huo, Mnzava alisema baada ya uchunguzi kubaini kuwa mfanyabiashara huyo alifuata taratibu zote za kisheria, ikiwemo kuandika maombi, kupimiwa eneo na kulipia ada ya Sh 900,000, serikali inatambua haki yake ya kutumia eneo hilo.
Baada ya kusikiliza pande zote, Mnzava alieleza kuwa mfanyabiashara huyo alifuata taratibu zote za kisheria, huku serikali ikiweka utaratibu wa kuwapatia wananchi hao eneo mbadala jirani bila gharama yoyote ili waendelee na shughuli zao.
Hata hivyo, kutokana na kundi la vijana wanaojiita ‘Sisi Kwa Sisi’ kuwepo katika eneo hilo kwa muda mrefu wakijipatia kipato, serikali imeamua kuwapatia eneo mbadala jirani bila kuwatoza gharama yoyote.
“Tutawapatia eneo lingine karibu na hapa bila kulipa hata shilingi moja. Eneo hilo liko ndani ya hifadhi ya barabara ambayo serikali ina mamlaka nayo, na TARURA watafanya utaratibu wa kuwapangisha rasmi,” alisema Mnzava.
Aidha, alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Afisa Mipango Miji pamoja na uongozi wa kampuni ya TPC kuhakikisha wanabainisha eneo lisilo na mgongano ili vijana hao waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Pasua, Barreh Ally Farrah, alisema alilazimika kufikisha suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya baada ya mgogoro kuwa mkubwa, ambapo hatua ya awali ilikuwa kusitishwa kwa notisi ya kuwaondoa wananchi.
Alisema uamuzi huo umezingatia hali kwa pande zote na kuendana na kauli mbiu ya Rais Samia Suluhu Hassan ya “Kazi na Utu”.
Aidha, diwani huyo alieleza kuwa Mkuu wa Wilaya ametumia busara kubwa kwa kusikiliza pande zote na kumaliza mgogoro huo kwa amani bila kutumia nguvu.
Baadhi ya viongozi wa kikundi hicho, akiwemo mwenyekiti Charles Makalakala pamoja na Bakari Juma na Silvanus Mtalisi, walimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuingilia kati na kutoa suluhu ya amani.
“Sisi tumekaa hapa kwa muda mrefu tukifanya biashara halali. Baada ya mfanyabiashara huyu kupewa eneo kisheria, alianza kututaka tuondoke bila mazungumzo. Tunashukuru serikali kwa kutusikiliza na kutoa uamuzi wa haki, nasi tumeukubali,” alisema Makalakala.
Kwa mujibu wa taarifa, kikundi hicho kina zaidi ya wanachama 80 waliokuwa wakitegemea eneo hilo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Awali akizungumza mfanyabiashara huyo Denis Somi alieleza kuwa uwepo wa shughuli za biashara katika eneo la hifadhi ulikuwa unakiuka matumizi yaliyokusudiwa na pia kusababisha changamoto za msongamano na usalama.
“Nilifuata taratibu zote kisheria kupata eneo hili, baada ya kulipia nikaruhusiwa kulitumia kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vya ujenzi na kurahisisha upakuaji wa mizigo,” alisema.
Awali, Januari 30 mwaka huu, Afisa Mtendaji wa Kata, Hidaya Mwantemi, aliwapa notisi ya siku saba wananchi waliokuwa wakitumia eneo hilo kuondoka ili kupisha matumizi mapya ya eneo hilo.
Hatua ya Mkuu wa Wilaya imeweka msingi wa kumaliza mgogoro huo kwa njia ya amani huku pande zote zikikubaliana na maamuzi yaliyotolewa.