MOSHI-KILIMANJARO.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa ugawaji wa miche ya kisasa ya parachichi katika Jimbo la Vunjo, Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Iddi Mfinanga, alisema hafla hiyo itafanyika Aprili 23 mwaka huu katika Kata ya Kilema Kusini, wilaya ya Moshi mkoani hapa.
Alisema katika tukio hilo, Katibu Mkuu atagawa jumla ya miche 100,000 ya parachichi kwa majimbo mawili ya Vunjo na Moshi Vijijini, ambapo kila jimbo litapata miche 50,000.
Mfinanga alieleza kuwa zao la parachichi ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayopewa kipaumbele, huku akihimiza wananchi kupanda angalau miche mitano kila mmoja ili kujikwamua kiuchumi.
Aliongeza kuwa kwa sasa mche mmoja wa parachichi unauzwa kwa shilingi 5,000, ambapo Serikali imetoa ruzuku ya shilingi 2,500 kwa kila mche, huku Wabunge wakigharamia usafirishaji wa miche hiyo kutoka mikoa ya Mbeya na Njombe.
Aidha, alisema soko la zao hilo linaendelea kukua kimataifa, likiwa na uhitaji mkubwa katika nchi za Ulaya kama Uingereza na Uholanzi, Asia katika nchi za China na India, pamoja na Afrika Kusini.
Alisisitiza kuwa bei ya parachichi ipo juu sokoni na inalifanya zao hilo kuwa na ushindani sawa na kahawa, hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kuchukua miche hiyo kwa ajili ya kuipanda.
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu bora barani Afrika katika uzalishaji wa parachichi zenye soko kubwa duniani, hasa aina ya Hass na Fuerte, hali inayochochea ukuaji wa sekta ya kilimo na uchumi wa taifa kwa ujumla.







