Mkazi wa Bonite Kata ya Shirimatunda Bw. Charles Chuwa, akiwa amebeba mbolea ya kukuzia mahindi, ambayo inatolewa na Serikali kwa ruzuku, hali ya upatinaji wa mbolea hiyo kwa sasa katika mji wa Moshi ni mkubwa.
MOSHI-KILIMANJARO.
JUMLA ya tani 2,200 za mbolea yenye kirutubisho cha naitrojeni, inayotolewa na Serikali kwa ruzuku, zimesambazwa katika wilaya za Siha, Hai na Moshi kwa lengo la kuwahudumia wakulima kwa bei elekezi.
Hayo yamesemwa Aprili 20,2026 na Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kaskazini, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upatikanaji wa mbolea ya kukuzia katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema kutokana na ongezeko la uhitaji wa mbolea katika msimu huu wa kilimo, hususan katika wilaya hizo tatu, mamlaka hiyo imelazimika kuleta tani hizo ili kuondoa uhaba uliokuwepo hapo awali.
Kwa mujibu wake, mbolea hizo zimesambazwa kupitia mawakala na vyama vya msingi vya ushirika, huku kiasi kilichobaki kikiendelea kuuzwa kupitia mawakala waliopo.
Aidha, amesema uwepo wa mbolea hiyo umewezesha wakulima wengi kuendelea kunufaika na ruzuku ya Serikali, akitoa rai kwa mawakala kuzingatia bei elekezi wanapouza bidhaa hiyo.
Akizungumzia Mkoa wa Arusha, hususan Wilaya ya Karatu, alisema zaidi ya tani 30 za mbolea zimepelekwa kwa wakulima, na kwamba hadi mwisho wa wiki hiyo zaidi ya tani 200 zinatarajiwa kuwa zimefikishwa wilayani humo.
Kwa upande wake, Afisa Udhibiti wa Ubora wa Mbolea nchini (TFRA), Kanda ya Kaskazini, Albert Mwaulambo, alibainisha kuwepo kwa changamoto kadhaa, ikiwemo baadhi ya wakulima kujaribu kununua mbolea kwa fedha taslimu bila kufuata utaratibu wa mfumo wa ruzuku.
“Baadhi ya wakulima wana dhana kuwa mbolea hizi zinauzwa huria, jambo ambalo si sahihi. Mbolea hizi zinatolewa kwa mfumo wa ruzuku, hivyo ni lazima mkulima awe amejiandikisha ili aweze kunufaika,” alisema.
Aliongeza kuwa wakulima wanapaswa kuacha kuchagua mbolea kwa majina badala yake waangalie virutubisho vilivyomo, akisisitiza kuwa mbolea zote zenye kiwango kikubwa cha naitrojeni zinafaa kwa kukuzia mazao.
“Wakulima wafike kwa mawakala wakiwa na vitambulisho vyao pamoja na fedha, hasa wale waliopokea ujumbe mfupi (SMS) unaowaruhusu kununua mbolea ya ruzuku,” alisisitiza.
Baadhi ya wakulima, akiwemo Peter Kweka na Charles Chuwa, walisema elimu inayotolewa na maafisa kilimo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea imeongeza uelewa na hamasa ya matumizi ya mbolea ya kukuzia, hali iliyochangia kuongezeka kwa mahitaji ya pembejeo hiyo.














