MASIJALA YA KAHAWA KUIMARISHA SEKTA NA UFUATILIAJI WA DATA NCHINI

MOSHI-KILIMANJARO.

UWEPO wa ofisi maalum ya masijala inayohusiana na sekta ya kahawa umeelezwa kuwa ni jambo muhimu katika kukuza sekta hiyo nchini, kwani utahakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi na za kuaminika kuhusu zao hilo muhimu la kibiashara.

Hayo yameelezwa hivi karibuni na Francis Kajiru kutoka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) wakati wa warsha ya wadau wa kahawa kutoka taasisi za umma na binafsi kuhusu usajili wa kahawa na kanzidata ya sekta hiyo, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Usajili wa shughuli zote zinazohusiana na sekta ya kahawa pamoja na usimamizi mzuri wa data ni muhimu sana, kwani hutumika kama uti wa mgongo katika kufuata kanuni za kimataifa na kuimarisha ufuatiliaji wa zao hilo kwa ujumla,” alisema Kajiru.

Aliongeza kuwa usajili unaosimamiwa na TCB ni hatua kubwa katika kufanya mnyororo wa usambazaji wa kahawa nchini kuwa wazi na unaoweza kufuatiliwa, hali itakayowawezesha wanunuzi kujua asili ya kahawa wanayonunua.

Kwa mujibu wa Kajiru, mfumo huo pia utatoa uhakika kwa wateja kwamba kahawa wanayonunua imezalishwa kwa kuzingatia sheria mpya, ikiwemo zile zinazozuia uharibifu wa mazingira kama ukataji wa miti.

Alifafanua kuwa Masijala Kuu ya Kahawa ya Tanzania ni mfumo wa kitaifa unaounganisha taarifa za wazalishaji na uzalishaji wa kahawa, ikiwa ni pamoja na mipaka ya mashamba, kwa lengo la kurahisisha ufuatiliaji, kuimarisha udhibiti na kusaidia upatikanaji wa masoko.

Kajiru alibainisha kuwa mfumo huo umetayarishwa kwa usaidizi wa Umoja wa Ulaya (EU), huku utekelezaji wake ukianza Juni 2025 hadi Aprili 30, 2026.

 Alieleza kuwa unatekelezwa na Muungano wa Kimataifa wa Masoko Yanayoibuka kwa kushirikiana na kampuni ya BizyTech, pamoja na msaada wa kiufundi kutoka Taasisi ya Misitu ya Ulaya.

Kwa upande wake, Mkuu wa Maliasili wa EU nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Lamine Diallo, alisema kuwa EU imejizatiti kusaidia mifumo ya kitaifa inayokuza uwazi, ufuatiliaji na uendelevu wa muda mrefu.

“Masijala Kuu ya Kahawa ya Tanzania ni mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa maendeleo ya sekta ya kahawa,” alisema Diallo.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.